Na Esther Macha,TimesMajira Online, Chunya
ZAIDI ya wakazi 10000 wa Kata ya Sangambi, wilayani Chunya katika Mkoa wa Mbeya, wanatarajiwa kupata huduma za Afya baada ya serikali kutoa sh milioni 316 kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya kwenye Kata hiyo.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Ntundu Chapa alipozungumza na timu ya waandishi wa habari wa mkoa wa Mbeya juzi amesema kwa sasa ujenzi wa kituo hicho cha Afya umekamilika kwa asilimia 85 na kwamba huduma za matibabu zinatarajiwa kuanza Juni mosi mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Chunya , Tamimu Kambona amesema maelekezo ya serikali kuwa kila halmashauri inayokusanya mapato ya ndani ya Bil.3 mpaka bil.4 iweze kujenga kituo cha afya kimoja lakini halmshauri hiyo iliamua katika vikao vyake kujenga kituo cha afya kimoja na pamoja na madarasa mawili kwa kutumia mapato ya ndani .
Akizungumza na timu ya waandishi wa habari waliotembelea eneo la kituo hicho afya cha Sangambi Kambona amesema kuwa mpaka sasa wametumia shilingi million.300 ambazo zinatokana na mapato ya ndani na kuwa sasa wanaenda awamu nyingine ya mwisho ambapo wametenga mil.40 ambayo inaenda kumaliza ujenzi wa kituo hicho.
Aidha Kambona amesema kuwa lengo la halmashauri kwa sasa ni kumaliza majengo yote ili kuweza kuwahamisha watumishi kutoka kituo cha zamani kituo hicho kianze kufanya kazi haraka ili kuwasaidia wananchi kupata matibabu.
“Kituo hiki tunarajia kianze kufanya kazi mwezi wa sita mwaka huu waanze kutoa huduma,lakini vifaa tiba vyote vitakuwepo kutokana na zahanati ya awali ambayo inaendelea kufanya kazi mpaka sasa wakati wananchi wakiendelea kusubiri kukamilika kituo hicho cha afya na kuwa bajeti ya mwezi wa saba wametenga kiasi cha fedha ili kuweza kununua vifaa tiba vingine vikiwemo vitanda vya wagonjwa”amesema Kambona.
Mkazi wa Sangambi Wilayani Chunya ,Fatuma Juma amesema kuwa hospitali ipo moja tu na kuwa huduma bado ni changa na haijaweza kuboreshwa vizuri .
Venance Mwambugi Mkazi wa Sangambi amesema wanashukuru ujenzi wa kituo cha afya kinaelekea ukingoni kukamilika kwani siku za nyuma walikuwa na zahanti ambayo ni ndogo hasa ukizingatia kata hiyo ina vitongoji vingi ambavyo vyote vinategemea zahanati hiyo na akina mama wajawazito walikuwa wanaenda kujifungulia hospitali ya wilaya Chunya kutokana na zahanati hiyo kuwa ndogo .
Mwambugi amesema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwasaidia kujenga kituo cha afya hivyo waliomba kituo hicho cha kukamilika mapema ili wananchi waweze kupata matibabu na akina mama wajawazito waweze kujifungulia katika kituo hicho cha afya badala ya kusafiri umbali mrefu.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa