November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hatuwezi kuacha kujali, chupa za plastiki zinaua bahari

Na Robert Okanda,TimesMajira Online

ZAIDI ya chupa 5,000 za maji zilizotumika, zinaonekana zikiwa zimeipamba nguzo kubwa za Kirumi.

Zimepangiliwa vyema huku zikiwa kana kwamba ‘zinasalimia’ Kila mtu anayeingia na kutoka kwenye lango la Klabu ya Afya ya Colosseum iliyopo Masaki, Dar es Salaam.

Chupa hizo zilizotengenezwa kwa utaalamu, ni matokeo ya mradi ulioasisiwa na Shafina Jaffer kuadhimisha Siku ya dunia.

Shafina ni msanii wa Kitanzania na ambaye sasa anasomea Shahada ya Uzamili ya Uchoraji katika Chuo mashuhuri cha Royal College of Art London, nchini Uingereza.

Kazi hiyo ya sanaa ya kunakishi kwa kutumia chupa zilizotumika chini ya mradi wa ‘Hatuwezi Kuacha Kujali’, ilimchukua miezi mitatu kukamilika.

Anaelewa kuwa akiwa katika matembezi kando ya Ufukwe wa Coco, alishuhudia chupa za plastiki zenye idadi isiyohesabika zilizotupwa kizembe katika ufukwe huo mzuri.

Alifikiria nguzo za baadhi ya majengo akaona chupa za plastiki zilizojaa ufukweni na ambazo ni takataka, zinaweza kutumika kwa ajili ya kunakishi. Alitekeleza wazo hilo.

Shafina anatoa wito kwa mighahawa katika eneo la Masaki na wakazi wa Dar es Salaam wasitupe chupa za plastiki zilizokwishatumika, badala yake zikusanywe na kufanyiwa matumizi mbadala kama alivyozikusanya yeye na kunakishi nguzo za ukumbi wa jengo la mazoezi.

Pia amewataka wakazi wa Dar es Salaam kufanya bidii zaidi kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Hotel ya Colosseum Shafina Jaffer akimalizia sehemu ya mradi kwa mojawapo ya nguzo za majengo ya mazoezi zilipo kando ya barabara ya Haole Sellassie Masaki mjijini Dar es Salaam hivi karibuni. (Na Mpigapicha )

Anasema uchafuzi wa plastiki umekuwa suala la kimataifa hali inayohatarisha sayari dunia.

” Wengi wa wakazi hutupa chupa tupu barabarani tu baada ya kunywa maji mvua zikinyesha husafirishwa na maji mpaka baharini na zinaweza kuwa na athari kubwa kwa mazingira,” anasema.

Takwimu za Programmu ya Mazingira ya Shirika la Umoja wa Mataifa (UNEP) nchini Tanzania zinaonesha kila mwaka, zaidi ya tani milioni 300 za taka za plastiki hutolewa huku kukiwa na ongezeko la asilimia tisa kila mwaka.

Zaidi ya hayo, asilimia 75 ya plastiki yote inayozalishwa inakuwa takataka na asilimia 91 ya plastiki yote haijasafishwa.

Takwimu hizi zinatisha ikizingatiwa kwamba inachukua hadi miaka 500 kwa chupa moja ya maji plastiki kuoza kawaida.

Katika sehemu ambayo ni nzuri kiasili kama Dar es Salaam, Shafina anaamini kwamba ni lazima kila mtu kuhakikisha anatimiza wajibu katika kuhifadhi asili.

Kwa mujibu wa UNEP, kila mwaka, wanyama milioni moja wa baharini hufa kutokana na uchafuzi utokanao na mabaki ya malighafi za plastiki.

Msanii huyu anasema bila maboresho ya udhibiti wa taka zaidi ya yale ambayo tayari yamefanyika sasa, tani milioni 99 za taka za plastiki zisizodhibitiwa zitaishia kwenye mazingira kufikia mwaka 2030.

“Ikiwa hatutadhibiti tatizo la uchafuzi wa plastiki katika bahari zetu, tunatishia kuchafua mtandao mzima wa chakula cha samaki na wanyama wengine baharini,” kutoka kwa phytoplankton (mmea wa baharini unaosaidia usafishaji wa maji yaliyochafuliwa).

Anasisitiza, ” Itakuwa tumechelewa sana wakati tutakapofikia hii hali na haitawezekana kurudi nyuma ili kubadilisha uharibifu uliosababishwa na uchafuzi wa mazingira yetu.”

Anasisitiza kuwa,kizazi cha watu wanaofahamu kanuni na taratibu za kimataifa, ni lazima kichukue hatua zinazohitajika ili kuunda ulimwengu ambao kila mtu anataka kuishi na anataka vizazi vijavyo viishi.

Uwepo wa binadamu katika ulimwengu huu haupaswi kuwa wa kulazimishwa na kutawaliwa na wasiwasi.

Usanifu wa sanaa ya Shafina utasalia katika Klabu ya mazoezi ya Colosseum hadi mwishoni mwa mwezi Mei, ambapo watu wanaweza kwenda kwenda na kuiona.

Sanaa hiyo inatumika kuwakumbusha na kuwahamasisha watu wote wanaopita katika ukumbi huo, umuhimu wa kutunza mazingira na kuwashawishi wapende kutumia vitu mbadala katika maisha ili kulinda uhai wa viumbe wengine.