Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imetekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan, alilolitoa jijini Dodoma Septemba 2021 kuhusu kuandaa mkakati kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini wa kupunguza utegemezi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Hayo yamesemwa Mei 09, 2022 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima wakati akifungua kikao cha wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa Kanda ya Mashariki kilicholenga kutoa maoni ya wadau hao katika kuweka mikakati ya kujisimamia na kupunguza utegemezi wa fedha za wafadhili.
Waziri Dkt Gwajima alisema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yamekuwa yakichagiza jitihada za Serikali kuwaletea Wananchi wake maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi ya afua mbalimbali zikiwemo za Afya, Kilimo, Elimu, Maji, Mazingira, Miundombinu, Utawala Bora, Nishati, hifadhi wa Jamii, Mifugo na Uvuvi, Uwezeshaji wa Jamii na Sekta nyingine mtambuka.
“Miradi hiyo, sio tu imewanufaisha Wananchi wetu kijamii, bali pia imechangia katika kuongeza ukuaji wa uchumi, kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza fursa za ajira hususan kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu” alisema Dkt Gwajima
Aliongeza kuwa Wizara inashirikiana na wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuandaa Mpango Mkakati wa kuyajengea uwezo Mashirika hayo ili kupunguza utegemezi na kuwa na uendelevu wa shughuli zao na utaratibu huo wa kukusanya maoni kutoka katika Mashirika hayo unafanyika katika Kanda tano ikiwemo Kanda ya Mashariki Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa.
“Wizara ilianza mchakato kwa kuandaa Mkakati huo, tarehe 10 Novemba, 2021, ambapo iliunda Kamati ya wajumbe 20 ikijumuisha wataalam kutoka Wizarani, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, sekta binafsi na Wadau wengine.” alisisitiza Dkt Gwajima
Aidha Waziri Dkt. Gwajima alisema Kamati iliyoundwa mpaka sasa imefanikisha kukamilika kwa andiko la majadiliano (consultation paper), nyenzo za ukusanyaji wa taarifa na maoni kutoka kwa wadau mbalimbali (stakeholders engagement tools), pamoja na ukusanyaji wa taarifa na maoni kutoka kwa wadau.
Amewaasa wadau na washiriki wa mkutano huo kutoa maoni yao yatakayosaidia kupatikana kwa Mkakati huo kwa kuzingatia umuhimu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika maendeleo na ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Pia Dkt Gwajima alitoa wito kwa wadau wengine kuendelea kuiwezesha Kamati katika shughuli nyingine zinazofuata ili kukamilisha mkakati huu utakaosaidia kukidhi malengo ya kuanzishwa kwa Mashirika yenu na matarajio ya jamii ya Watanzania.
“Nitoe shukrani zangu za dhati kwa Bw. Laurence Wilkes kwa niaba ya FCDO ya Ubalozi wa Uingereza, kwa kuiwezesha Kamati kufanya mikutano hii ya kukusanya maoni katika Kanda zote tano zinazoendelea” alisema Dkt Gwajima
Naye Mkurugenzi wa Shirika la CBM International na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha kuandaa Mkakati huo Nensia Mahenge alisema Kikosi hicho kinaendelea kukusanya maoni kwa ajili ya ya kutengeneza Mpango Mkakati kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyopo nchini kuweka mikakati ya kujitegemea na kuwa na uendelevu katika utekelezaji wa majukumu na miradi mbalimbali kwa wananchi.
“Kwa kuanzia Kikosi kazi chetu kilifanikiwa kukusanya maoni katika Kanda ya Ziwa iliyohusisha Mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara na baada ya mkutano huu Kamati itaendelea na kukusanya maoni katika Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za Juu na kumalizia Kanda ya Kati” alisema Nensia
Kwa upande wake Bw. Laurence Wilkes kwa niaba ya FCDO ya Ubalozi wa Uingereza amesema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni wadau muhimu katika maendeleo ya Taifa kwani yakishirikiana na Serikali kwa ukaribu itasaidia kuendelea kutoa huduma zilizo na uhakika na muendelezo kwa wananchi
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â