November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UNFPA kuchagiza usawa wa jinsia nchini

NJa Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imekubaliana na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA) kushirikiana kutafuta namna na mbinu bora zitakazoiwezesha Tanzania kuzingatia misingi ya Usawa wa kijinsia.

Makubaliano hayo yamefikiwa (Aprili 06, 2022) Jijini Dar Es Salaam wakati wa Kikao kati ya Wizara na Wadau wa Maendeleo kuhusu masuala ya Usawa wa Kijinsia kutoka UNFPA.

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula amesema, Tanzania itahakikisha masuala yote kuhusu usawa wa kijinsia yanazingatiwa kwa kuwapa fursa wanawake katika Nyanja mbalimbali zikiwemo za uongozi na kiuchumi.

” Tunaongozwa na Miongozo mbalimbali ikiwemo Dira ya Taifa …..na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025, hivyo, niwaombe tu, tuzingatie haya kwenye mipango yetu Shabaha ni twende pamoja kwa matokeo chanya na ya haraka” alisema Dkt. Chaula

Amesema jukumu kubwa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni kushirikiana na Serikali kutatua changamoto zinazoikabili jamii ikiwemo ukatili wa kijinsia unaozidi kushamiri.

” Tunasikia kila siku ukatili, mauaji sasa tushirikiane tuweke nguvu ya pamoja, tuwekeze katika elimu kwa jamii, hii itasaidia kuondokana na vitendo vya ukatili ” alisema Dkt. Chaula

Akichangia mada wakati wa kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju amesema, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau kutafuta suluhu ya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Kwa upande wake Mshauri wa masuala ya Kijinsia kutoka UNFPA Maja Hansen amesema Shirika hilo liko tayari kushirikiana na Wizara katika utekelezaji wa Mipango mbalimbali ikiwemo Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) 2017/2018-2021/2022.

Mkutano kati Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na UNFPA ni muendelezo wa vikao vya majadiliano na wadau mbalimbali kwa lengo la kutatua changamoto za jamii.

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt Zainab Chaula akizungumza na Wawakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA) katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar Es Salaam tarehe 06/04/2022.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju akichangia Jambo wakati wa kikao cha Wizara na Wawakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA) kwenye Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar Es Salaam tarehe 06/04/2022.
Mshauri wa masuala ya Kijinsia kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA) Maja Hansen akimueleza Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula vipaumbele vya Shirika hilo alipotembelea ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam tarehe 06/04/2022.
Baadhi ya Wakurugenzi na Maafisa wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika kikao na Wawakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA) katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam tarehe 06/04/2022.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA) mara baada ya kikao kati ya Wizara na Shirika hilo kilichofanyika Jijini DSM (kushoto/Kulia)