November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lishe duni inavyoathiri ukuaji wa mtoto

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

Wazazi/walezi wameaswa kuzingatia suala la lishe bora kwa watoto ili kuepuka athari za lishe duni ukiwemo utapiamlo na udumavu  kwa mtoto na hatimaye kuathiri ukuaji wake.

 Kwa mujibu wa utafiti kutoka TDHS-MIS,kutokana na maboresho yaliyoonekana kwenye taratibu za lishe kwa watoto wachanga na watoto wengine wadogo ni pamoja na unyonyeshaji na lishe ya vyakula vya ziada kuwa ni sababu muhimu zilizochangia katika kupunguza kiwango cha udumavu kitaifa kutoka asilimia 34.7 mwaka 2015 /16 hadi asilimia 31.8 mwaka 2018.

Aidha tafiti zinabainisha kuwa licha ya maboresho hayo jamii inapaswa kutambua kuwa udumavu mkali bado unaathiri mtoto mmoja kati ya watoto kumi wenye umri wa chini ya miaka mitano nchini kote .

Akizungumza jijini hapa,Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya Japhet Msoga amesema,lishe duni kwa mtoto husababisha  changamoto mbalimbali za Utapiamlo kama vile ukondefu, udumavu wa kimwili na kiakili,  upungufu wa madini na vitamin.

Aidha amesema, lishe duni husababisha kupungua kwa kinga ya mwili hivyo kuongeza uwezekano wa kupata maambukizi ya Magonjwa.

“Lishe duni katika miaka miwili ya mwanzo ya maisha ya  mtoto inaweza kuathiri ukuaji wa viungo na ubongo na utapiamlo kwa mtoto na madhara yake yasiweze kurekibishika tena maishani mwake..,hivyo,husababisha uwezo wa mtoto wa kujifunza kuwa chini na hata kuathiri utendaji wake wa kazi hata atakapokuwa mtu mzima”amesema Japhet na kuongeza kuwa

“Ulaji wa mtoto kuanzia miaka miezi  0 hadi 6 amesema, mtoto anatakiwa kunyonya maziwa ya mama pekee bila chakula kingine chochote…,anapofikia umri wa Miezi 6  mahitaji ya mwili ya virutubisho huongezeka, hivyo maziwa ya mama pekee hayawezi kutosheleza mahitaji yake ya kilishe.”

Amesema,katika umri huo mtoto anapaswa aanze kupewa chakula cha ziada kwa kuzingatia makundi matano ya chakula huku akiendelea kunyonya maziwa ya mama hadi atakapofikisha umri wa miaka miwili ambapo atachishwa maziwa ya mama na kuendelea  kula mlo kamili wa familia kwa kuzingatia makundi matano yote ya chakula hadi  atakapofikia umri wa miaka minane na kuendelea.

Makundi ya vyakula yanayokamilisha mlo kamili ambao pamoja na watu wengine lakini pia mtoto mdogo anapaswa kuandaliwa mlo kamili

“Lishe bora ni hali inayotokana na kula mlo kamili na wakutosha wenye mchanganyiko wa vyakula kutoka katika makundi matano ambayo Nafaka, Asili ya wanyama na jamii ya mikunde, Mbogamboga ,Matunda na  Asali na Mafuta.”

“ Inashauriwa mtoto na jamii kwa ujumla kula angalau chakula kimoja kutoka katika kila kundi la chakula katika kila mlo.

Kwa upande wake Mkazi wa Dodoma Ben Bago amesema moja ya changamoyo inayowakabili Wazazi/walezi wengi ni kutokuwa na uelewa kuhusu masuala ya lishe na umuhimu wake.

Aidha amesema,asilimia kubwa ya wazazi /walezi hawawajibiki ipasavyo katika suala zima la malezi na makuzi ya watoto wao hasa katika suala la lishe lakini pia alisema kuna mkanganyiko wa watoa huduma za afya kuhusu maana ya lishe bora.

Kwa upande wake mdau wa masuala ya lishe kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Mimi ni Taa ya jijini Dodoma Dorcas Shayo amesema,kumekuwa na changamoto ya masuala ya lishe kwa watoto kutokana na jamii kubwa kukosa elimu ya lishe.

“Kuna mwananchi ambaye alifiwa na mtoto kutokana na ukosefu wa lishe,lakini ndani alikuwa na mazao ya kila aina lakini hakuwa na elimu ya namna ya kuyatrumia yale mazao kwa ajili ya kuandaa chakula cha mtoto.”amesema Shayo

Ameiomba Serikali kupitia maafisa lishe wake kutoa elimu ya kutosha kwa wazazi ,walezi na wananchi kwa ujumla ili kuwanusuru watoto na ukosefu wa lishe na kuwasababishia udumavu na utapiamlo.