November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yakoshwa na kasi ya ujenzi na ubora maabara Changamani TAEC

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Tume ya Nguvu ya Atomiki Tanzania kwa kutekeleza Mradi wa Ujenzi wa Maabara Mchanga mano awamu ya pili kwa ufanisi.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo baada ya kutembelea Mradi huo Jijini Arusha Kaimu Mwenyekiti Mhe. Alyoce Kamamba (Mb) amesema hatua ya utekelezaji wa mradi huo ni nzuri na inaridhisha na thamani ya fedha iliyowekezwa inaonekana.

Mhe. Kambamba amesema Kamati hiyo ipo tayari kutoa ushirikiano kwa Tume hiyo ili ifanye shughuli zake kwa weledi na ufanisi, huku akiitaka kufanya utafiti wa namna ya kuangamiza mbu wa malaria nchini kama walivyoweza kufanikiwa kuangamiza mbugu zanzibar.

” Mradi wa Ujenzi wa Maabara hii unaridhisha sana ukiangalia unaona kabisa thamani ya fedha iliyotumika hapa, sisi tuwaahidi ushirikiano wa kuwawezesha kufanya kazi zenu kwa ufanisi,” amesema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) amesema katika kuhakikisha nchi inakuwa na wataalam wengi katika nyanja za Sayansi, Serikali imeanza kuwekeza katika kuwaandaa wataalam wengi zaidi kwa kutoa ufadhili wa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi kidato cha sita kwenda kusoma nje ya nchi.

“Tayari nilishawaelekeza Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania kutenga fedha kwa ajili ya kutoa ufadhili wa masomo ili kuwa na wataalam wengi, jambo ambalo wamenijulisha kwamba wameshaanza utekelezaji kwa kutenga fedha hizo, ” amesema Waziri

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, Prof. Lazaro Busegela ameiambia Kamati hiyo kuwa ujenzi wa Mradi huo wenye ofisi na maabara za kisasa kumi umefikia asilimia 94 na kwamba unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu kulinga na mkataba.

Profesa Busegela ameongeza kuwa mpaka sasa tayari Malipo ya ujenzi wa Maabara Changamano awamu ya pili yameshafanyika baada ya mkandarasi kuwasilisha hati za madai (certificates) na hadi sasa mkandarasi amewasilisha hati 14 za madai ambapo malipo kwa hati zote 14 zenye Jumla ya shilingi 7,859,996,178 yameshafanyika ambayo ni sawa na asilimia 75.57 ya mkataba.

Aliongeza kuwa kati ya fedha hizo Shilingi 3,641,922,344.22 ni ruzuku kutoka Serikalini na Shilingi 4,217,468,833.88 ni mapato ya ndani.