Na Heri Shaaban, TimesMajira Online, Dar es Salaam
TAASISI ya Wahenga Aluminium imetoa Sh 500,000 kusaidia kikundi cha kikoba cha Tujijenge Pamoja kilichopo Kata ya Minazi Mirefu ili kiweze kujikwamua kiuchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa Wahenga Aluminium, John Ryoba, alichangia fedha hizo katika harambe ya kuadhimisha miaka mitano ya kikundi hicho ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba aliyechangia Sh 100,000 na kuahidi kutoa mchango mwingine baadaye.
Akizungumza katika hafla hiyo Ryoba ambaye alikuwa mgeni maalumu alisema amekuwa akishirikiana na kikundi hicho pamoja na kuchangia shughuli mbalimbali za chama.
“Niko pamoja na ninyi na nitaendelea kuwasaidia ili mjikwamue kiuchumi kwa sababu tunaamini wanawake mnaweza,” alisema Ryoba.
Aliwataka wanachama wa kikoba hicho kushirikiana kwa pamoja ili waweze kusonga mbele na kufikia malengo yao.
Kwa upande wake mgeni rasmi Mwenyekiti wa CCM Mkoa Dar es Salaam, Kate Kamba, alisema chama kitashirikiana nao katika kutatua changamoto zao na kuwasaidia ili waweze kusonga mbele.
Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Segerea, Rutha Rucharaba, alisema Kata ya Minazi Mirefu kuna vikundi vingi vya wanawake na vijana lakini havijapata mikopo inayotolewa na halmashauri.
Alisema hawajajua kinachokwamisha hali hiyo na changamoto hiyo na kuomba CCM Mkoa wa Dar es Salaam iweze kuwasaidia.
Rutha alisema awali Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonah Ladslaus Kamoli, alichangia bati 20 kwa ajili ya ofisi inayojengwa na kikundi hicho.
Wenginge waliochangia harambee hiyo ni Madiwani Wanawake wa Wilaya ya Ilal ambapo Lucy Lugome wa Kisukuru alichangia Sh100,000, Rukia Chacha (Sh 100,000) na Moza Mwano ambaye pia ni mlezi wa kikoba hicho (Sh 100,000), UWT Minazi Mirefu (50,000) na
Msaidizi wa Mbunge (Sh 30,000).
Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake Tujijenge Pamoja, Hadija Magube, alisema wanakabiliwa na changamoto za viti 300, meza 60, maturubai sita, vifaa vya ofisi na umaliziaji wa ofisi yao ambapo vyote vinagharimu Sh milioni 21.4.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili