Na Judith Ferdinand, Mwanza
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka wataalam, wavuvi na wafugaji wa viumbe maji kulinda rasilimali za uvuvi ili kustawisha uchumi wa bluu.
Naibu Waziri Ulega ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa mwaka wa kimataifa wa uvuvi mdogo na ukuzaji viumbe maji – IYAFA 2022 uliofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza.
Ulega amesema upo umuhimu wa kuanzisha chombo cha ulinzi wa rasiliamli za uvuvi chenye wataalam wa uvuvi na ulinzi ili kuhakikisha rasilimali hizo zinalindwa.
Amesema,Serikali ya awamu ya sita imeweka malengo ya kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinalindwa ili kustawisha uchumi wa bluu utakaosaidia kukuza pato la wavuvi, wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi na taifa kwa ujumla.
“Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikisikia changamoto nyingi zinazowakabili wavuvi na rasilimali za uvuvi,sasa ni wakati muafaka wa kukabiliana na changamoto hizo,” amesema Ulega.
Hivyo Ulega aliwataka watumishi wa Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) waone ni namna gani wanaweza kusaidia sekta ya uvuvi kwa baadhi ya maeneo hususani changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo nchini.
Pia aliwataka wataalam wa sekta ya uvuvi kushirikiana na wawakilishi wa FAO kuandaa mradi kwa ajili ya matumizi bora ya Ziwa Victoria utakaosaidia katika kuepusha migogoro na wavuvi na utakaolinda rasilimali za uvuvi.
Aidha amesema,wataalam waandae mradi utakaosaidia katika kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi kwa kuwa bado ipo changamoto ya upotevu wa mazao hayo.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa FAO hapa nchini, Charles Tulahi amesema Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limetangaza mwaka 2022 kuwa ni mwaka wa uvuvi mdogo na ufugaji viumbe maji kutokana na mchango mkubwa ambao sekta za uvuvi na ufugaji wa viumbe maji zinatoa katika kuimarisha lishe, kutokomeza umaskini na katika kuongeza ajira.
FAO imepewa jukumu la kuongoza maadhimisha ya mwaka huu wa uvuvi mdogo na ufugaji wa viumbe maji kwa kushirikiana na serikali mbalimbali duniani, mashirika pamoja na vyombo muhimu kwa wavuvi. Tulahi ameipongeza Tanzania kwa kuwa na Mpango kazi wa Kitaifa wa utekelezaji wa miongozo ya uvuvi nchini.
Kabla ya kuzindua maadhimisho hayo, Naibu Waziri Ulega alitembelea mwalo wa Kirumba ambapo aliwaeleza wavuvi kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imepanga kuhakikisha tozo zote kichefuchefu zinaondolewa ili wavuvi na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi waweze kufanya shughuli zao kwa uhuru na tija zaidi.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â