Mwandishi Wetu,TimesMajira,OnlineDar
WANAWAKE jasiri kimaisha na kiuongozi wanapaswa kuandaliwa tangu utotoni, wakiwa shule ya msingi, sekondari na vyuo kimaadili na kielimu.
Hayo yameelezwa na jopo la wanawake wa Asasi ya Wanawake ya Maisha Bora Tanzania (TWBFG) waliotembelea watoto wa kike na kuwapa msaada wa taulo za kike wa Shule ya Msingi Kigezi iliyopo Chanika wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam.
Mmoja wa kinamama hao, Elitha Kahembe amesema wanawake wengi waliopata mafanikio kimaisha kama vile Rais Samia Suluhu Hassani, Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson walizingatia maadili na kujibidisha kielimi tangu utotoni.
“Si mnataka muwe viongozi kama Rais wetu, Samia? (wanafunzi wanapaza sauti: Ndiyoo!) Spika wa Bunge?” (Ndiyoo!). Basi zingatieni kusoma kwa bidii na kuwa na tabia nzuri kwa kuepuka kudanganywa na vijana ili kufanya mapenzi,” ameonya.
Kahembe amesema wakijihusisha na vitendo vya ngono wakiwa wadogo wanakuwa katika hatari ya kupata mimba za utotoni jambo ambalo linaweza kuzima ndoto za maisha walizojiwekea.
TWBFG walifanya mkutano maalumu na wanafunzi wa kike 241 ambao wamefikia umri wa kupevuka ili kuwaelimisha mambo mbalimbali muhimu kwa maisha yao ya baadae na namna ya kuhudhuria shule hata nyakati zao za hedhi.
“Tumekuja kuwaelimisha pia namna ya kutumia taulo za kike ili kuepuka kujificha nyumbani unapokuwa katika siku zako za hedhi,” amesema Mweka Hazina Msaidizi wa TWBFG, Lydia Maeda.
Mbali na kuwaelemisha juu ya namna ya kutumia tauolp hizo, aliwaelekeza namna ya kuwa wasafi na kuendelea na shughuli zao za kawaida pasipo hofu wawapo kwenye siku zao za hedhi.
Mweka hazina TWBFG, Leonida Lwekamwa aliwahakikishia wanafunzi hao kuwa Asasi yao ipo kwa ajili ya kuhakikisha wanawasaidia kwa namna mbalimbali ili wawe wanawake jasiri na wenye maisha bora katika maisha yao.
“TWBFG katika moja ya malengo yake ni kushirikiana na Serikali ili kuboresha maisha ya Watanzania kiafya, kielimu, kiuchumini ili kujenga jamii inayoishi maisha bora,” amesema Lwekamwa.
Amesema jamii ya Chanika ina bahati kwa sababu TWBFG imelenga kujenga ofisi ya makao makuu katika kata hiyo ya Chanika.
Amesema asasi hiyo imelenga kutoa elemu ya afya ya uzazi kwa jamii na kuielimisha juu ya kuepuka magonjwa mbalimbali yakiwamo kifua kikuu na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Mwanamama, Elizabeth Kaijage ameeleza majukumu ya TWBFG ni kuyasaidia makundi ya jamii yaliyopo kwenye mazingira magumu kama vile yatima, wajane, jamii inayoishi katika mazingira magumu na kutunza mazingira.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu kwa Umma ya Magonjwa Yasiyoambukiza (TOANCD), Leon Bahati ambaye alikaribishwa kwenye mafunzo hayo aliwatahadharisha kuwa kuna uhusiano kati ya magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyoambukiza.
“Ukiambukizwa magonjwa ya zinaa unaweza kujikuta anapata saratani ya kizazi, hata shingo ya kizazi na hata kuwa mgumba. Hivyo ni vizuri kuzingatia kutojihusisha na vitendo vya ngono,” amesema Bahati.
Pia amewahadharisha kuacha taiba ya kula vyakula vyenye wingi wa sukari, mafuta na chumvi ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza kama vile matatizo ya meno, shinikizo la damu, kisukari na uzito kupita kiasi.
Wanafunzi hao walieleza changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni uchache wa matundu ya choo, ukosefu wa maji, sehemu za kutupa taulo za kike zilizotumika na baadhi yao hukaa chini madarasani kwa kukosa madawati.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigezi, Selemani Kyumbo amesema ofisi yake ina taarifa za changamoto hizo hivyo atajadiliana na TWBFG pmaoja na wafadhili mbalimbali kuona ni namna gani watatatua matatizo hayo.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Tutela Lutinaa amesema shule hiyo itaendelea kushirikiana na TWBFG ili kuendelea kuwakuza kimaadili wanafunzi hao na kuwajengea uwezo wa kujiamini.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi