November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kukua kwa teknolojia kumerahisisha utoaji huduma kwa MWAUWASA

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Kukua kwa teknolojia kumesaidia na kurahisisha hupatikanaji na utoaji wa huduma ambapo watoa huduma uwafikia wateja kwa muda mfupi huku wapokea huduma wakipata huduma kwa haraka.

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), ni miongoni mwa watoa huduma ambao teknolojia imewasaidia kurahisisha katika utendaji kazi wao.

Akizungumza na majira/ timesmajira online, ilipomtembelea ofisini kwake jijini Mwanza,Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA Mhandisi Leonard Msenyele,anaeleza namna ambavyo kukua na kubadilika kwa teknolojia ilivyoweza kurahisisha utoaji wa huduma zao kwa wananchi.

Mhandisi Msenyele, amesema MWAUWASA wana dhamana ya kuhakikisha watu wa Mwanza na watu wanaoingia katika Jiji la Mwanza wanapata huduma ya maji safi na salama na kwa wakati unaotakiwa.

Amesema,ni kweli kumekuwa na teknolojia ambayo sasa hivi inakua kwa kasi sana,imerahisisha katika nyanja nyingi mfano katika suala la mawasiliano yao na wateja zamani ilikuwa ni lazima mteja aweze kufika katika ofisi zao ikiwemo ofisi kuu au za Kanda.

Lakini kwa sasa hivi mteja halazimiki kufika katika ofisi zao badala yake atafanya mawasiliano kwa njia ya simu ambapo anaweza kutuma ujumbe na kuwasilisha changamoto yake ambayo wataitatua kwa wakati kulingana na ukubwa.

Ameeleza pia inapotokea hitilafu katika mitambo yao ya maji wanawapa taarifa wateja wao kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno katika simu za wateja wao badala ya kupita na magari ya matangazo kutangaza.

“Maana awali tulikuwa na utaratibu wa kutumia magari kwenda mtaa kwa mtaa kutangaza ili wananchi wapate taarifa lakini sasa hivi kama kuna hitilafu katika mitambo yetu tunaweza kuwafikia wateja kwa ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu kwa kuwapa taarifa hiyo na kuwajulisha juu ya hitilafu iliopo,”amesema Mhandisi Msenyele na kuongeza kuwa

“Tunatumia majukwaa ya mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram, Facebook vile vile WhatsApp ambayo sasa hivi kuna vikundi ambavyo unaweza kutuma ujumbe wako na ukawafikia watu kwa urahisi zaidi,kuliko kwenda kwa mtu mmoja mmoja kwenye familia,”.

Pia ameeleza kuwa kwa kiasi kikubwa wamekuwa na urahisi sana wa kuwasiliana na wateja wao pindi inapotokea dharura ambapo wanaweza kuwafikia ndani ya muda huo huo watu wengi kwa mara moja tofauti na zamani walikuwa wanalazimika kwenda mtaani kumueleza mtu mmoja mmoja au kutangaza kwa kutumia magari.

Ambapo hali hiyo nayo ili kuwa ni changamoto kidogo kwani wanaweza kwenda upande mwingine mwa mji lakini huku kwingine hawajapata taarifa.

Lakini kwa sasa hivi wanaweza kuwa wamewafikia wateja kwa asilimia kubwa kwa muda mfupi sana.

Aidha ameeleza suala la pili ambalo teknolojia imesaidia ni ukusanyaji.na ulipaji wa ankara za maji.

Mhandisi Msenyele anaeleza kuwa zamani mteja alikuwa ana lazimika kulipa ankara ya maji katika ofisi za MWAUWASA za Kanda.

Ambapo mteja alilazimika kupanga mstari ili kuweza kufikia dirishani kwa mtunza fedha wao (cashier) kwa ajili ya kufanya malipo ya ankara za maji ,lakini kutokana na kukua kwa teknolojia kumekuwa na mabadiliko makubwa.

“Sasa hivi mteja alazimiki kuja kwenye ofisi zetu kwa ajili ya kulipa ankara za maji badala yake anaweza akalipa popote alipo iwe ni nyumbani hata kama anasafiri yuko nje ya Mwanza anaweza kulipa kupitia huduma za kifedha za mitandao ya simu hata benki ambayo nayo siku hizi wameturahisishia,kwani mtu anaweza kulipa kupitia simu yake endapo atakuwa amejiunganisha na huduma za simu benki,”amesema Mhandisi Msenyele.

Aidha amesema,kukua kwa teknolojia ambayo inawezesha mteja kulipa ankara za maji kwa kutumia simu zao za mkononi imesaidia kuondoa msongamano katika ofisi zao.

Pia imerahisisha muda kwa maana kwamba mteja anaweza kuwa na shughuli zake lakini anaweza akabonyeza simu mambo ya kulipa yakawezekana huku akiendelea na shughuli zingine.

Alazimiki kuchukua muda mrefu mpaka kwenda kwenye ofisi ndio maana ametolea mfano kuwa mteja hata akiwa nje ya Mwanza alazimiki kuja ofisini kama zamani ilivyo kuwa mtu akimtaka kupata au kulipa kulipia ankara ya maji ni aidha atume mtu au yeye mwenyewe afike kwenye ofisi zao.

“Lakini mwisho wa siku teknolojia imeturahisishia sana katika kuhakikisha kwamba watu wanafanya mambo mengi kwa wakati mmoja badala ya kuja kusimama kwenye ofisi zetu una weza kulipa huko huko ulipo na mfumo unakubali hivyo imerahisisha mteja kulipa ankara za maji,” ameeleza.

Mbali na hayo ameeleza kuwa kwa sasa wanaangalia suala la mita za maji ambazo wakimfungia mteja atakuwa anaingiza tu token anapo taka alafu maji yanafunguka.

“Tunahama kutoka kwenye mita zetu za kawaida hadi kwenye mita kama za wenzetu tanesco za luku ila sisi tutakuwa na mita za lipa maji kadri utumiavyo,naamini nayo ni sehemu ya teknolojia ambayo itatusaidia kuhakikisha sasa mteja haangaiki tena au kukatiwa maji kwa sababu labda amejisahau ajapata au ajalipia ankara ya maji,”amesema Mhandisi Msenyele.

Amesema,mita hizo mfumo wake utakuwa sawa na kununua bando kwa ajili ya matumizi ya simu linapo isha huduma inakataa atakapo lipia huduma inaendelea,kwaio ananunua token maji yanajifungua moja kwa moja ambapo hata wao watoa huduma itawarahisiashia kuto pambana na wateja kwenda kuwakatia maji suala ambalo mara nyingi linakuwa ni kero.

‘Mita hizi zitarahisisha huduma kwetu sote kwani mteja mwenyewe atakuwa na nidhamu kwa sababu maji yakikatika anaweza kuingiza token alafu maji yakafunguka moja kwa moja (automatically),tunaona namna ambavyo teknolojia itakuwa imeweza kutusaidia,” na kuongeza kuwa

“Ingawa bado hatujaenda sana tulikuwa na mradi wa majaribio hata kama haukuonesha mafanikio sana,suala la teknolojia limepanda kwa sababu teknolojia ya mita zile ilikuwa ni za 2G na sasa hivi tupo kwenye 4G na 5G,kwaio tunahama tunakwendwa kwenye teknolojia ya 4G na 5G kurahisisha wateja wetu kulipa muda wowote na maji wanakuwa wanajilipia kwa kadri wanavyokuwa wanatumia,”.

Kwa upande wake mmoja wa wananchi wa mtaa wa Nyamanoro Mashariki wilayani Ilemela,Lydia Hugo amesema suala la kukua kwa teknolojia kumewarahisishia hupatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwemo ya maji na mawasiliano.

Hugo amesema kwa sasa ikitokea maji yamekatika bila wao kupewa taarifa ya kwanini maji hayatoki wanawapigia simu moja kwa moja MWAUWASA na kuwaeleze shida zao kisha watoa huduma hao wanawapatia maji ya kwanini maji hayatoki.

Ameeleza kuwa kuna muda unakuta bomba kubwa linalowasambazia maji hadi kwenye nyumba zao limepata hitilafu limepasuka hivyo ili kuzuia upotevu wa maji wanawapigia MWAUWASA wanakuja mara moja kufanya marekebisho na huduma inarejea kama kawaida.

“Niseme tu kuwa teknolojia imeturahisishia sana hupatikanaji wa huduma ikiwemo suala la ulipaji wa ankara za maji,mimi uwa nalipa kupitia simu huku nikiwa na endelea na shughuli zangu bila ya kufika katika ofisi zao,pia naweza kuangalia deni la maji na daiwa kiasi gani na wakati mwingine MWAUWASA uwa wanatumia ujumbe kwa ajili ya kutukumbusha kulipa maji,” amesema Hugo.