November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri Mwakibete atoa maagizo TAZARA

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Kufuatia changamoto ya malimbikizo ya madeni kwa wastaafu na wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia TAZARA , Mkoa wa Tanzania, Naibu Waziri wa ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakibete ameuagiza uongozi wa shirika hilo kupeleka kiasi Cha shilingi Milioni mia mbili kila mwezi ili kuweza kutatua changamoto hizo

Akizungumza na waandishi wa Habari Jana Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kutembelea Taasisi mbalimbali zilizokuwepo chini ya Wizara ya ujenzi na Uchukuzi, Naibu Waziri huyo alisema changamoto kubwa ni juu ya maslahi ya watumishi kwa ujumla;

“Changamoto kubwa ni maslahi ya watumishi, kwa watumishi waliostaafu ambao michango yao ilienda kwenye taaissi za mifuko ya Jamii kama PSSF na NSSF lakini pia maslahi ya matumishi kwa maana ya wale ambao wameenda likizo”

Aidha Naibu Waziri huyo alisema wataunda tume maalumu ili kusikiliza changamoto zote zilizopo TAZARA na kuzifanyia kazi;

“Nitaenda kuongea na Mhe. waziri mwenye dhamana ya Wizara hii Prof. Makame Mbarawa pamoja na Katibu Mkuu tuunde timu maalumu itkayokuwa kazi yake kubwa ni kusikiliza changamoto za TAZARA na kuzitatua kwasababu tazara Ina changamoto nyingi sana”

Pia Atupele aliishukuru serikali kwa kuilipa TAZARA upande wa watumishi Tanzania;

“Naishukuru serikali kwa kuchukua wajibu wa kuilipa TAZARA upande wa watumishi Tanzania kwa maana kwamba kila mwezi tunalipa kutoa serikalini Bilioni moja na Milioni mia mbili na uhitaji ni Bilioni moja na Milioni miasita hivyo Milioni mianne wanatafuta kama mamlaka”

Naye Meneja Mkuu TAZARA Tanzania ,Fuad Abdallah alizitaja changamoto walizokuwa nazo katika Mamlaka hiyo kuwa ni uchakavu wa miundombinu, upungufu wa ingini na mabehewa

Fuad aliongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa Reli ya TAZARA mwaka 1976 ikiwa na ingini 102 leo hii ina ingini 14 hivyo changamoto kubwa sana ni vitendea kazi

Aidha alisema kufuatia serikali ya Tanzania na Zambia kuwa kwenye mchakato wa kubadilisha sheria ya awali ametaja vitu ambavyo vinatakiwa vifanyiwe maboresho ili Kuwepo na ushindani wa kibiashara;

“Miongoni mwa vitu ambavyo vinatakiwa vifanyiwe maboresho makubwa kwenye sheria ni pamoja na treatment ya uwekezaji katika umiliki wa Shea kwasababu umiliki wa zamani unazungumzia TAZARA inamilikiwa kwa hisa ya asilimia 50 kwa 50 kati ya nchi 2 lakini hausemi mmoja kati ya wawili akiwekeza inaathiri vipi hisa za mwingine”