Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Arusha
JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limewataka wananchi kutoa ushahidi Mahakamani wanapohitajika kwani kesi nyingi huaribika kutokana na kukosekana kwa ushahidi, jambo ambalo linasababisha kesi nyingi kupoteza kwa haki.
Wito huo umetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi ACP Justine Masejo mapema leo wakati akikabidhiwa Kituo cha Polisi Kisongo kilichojengwa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa IRMCT Arusha.
Masejo amesema, “kumekuwa na changamoto ya kesi nyingi mahakamani kuharibika kwa kukosekana ushahidi jambo ambalo linasababisha washtakiwa wanaokamatwa kuachiwa huru na kuendelea kutamba mitaani.”
Pamoja na wito huo, Masejo ameishukuru Taasisi ya Umoja wa Mataifa kwa kujenga kituo hicho ambacho kinakidhi vigezo na masharti ya kituo kidogo cha Polisi
Msaidizi Msajili wa Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa ya IRMCT, Horesa Bale Gaye amesema Umoja wa Mataifa kupita taasisi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mambo mbalimbali hususani maendeleo katika jamii.
“Tunashukuru ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na Jeshi la Polisi uliokuja na wazo la kujenga kituo cha Polisi Kisongo, ambapo awali kituo kilichokuwa kinatumika ni cha Uwanja wa Ndege wa Kisongo,” alisema Gaye.
Naye Mkuu wa Usalama wa IRMCT, All Hammood, amesema kuwa timu ya usalama ya Umoja wa Mataifa iko tayari kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufanya kazi pamoja na Jeshi la Polisi nchini.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kushuhudia ufunguzi huo, wameishukuru taasisi hiyo ya umoja wa Mataifa kwa kuwajengea kituo cha kisasa katika eneo lao la Kisongo ambacho wamesema kitakuwa mwaarobaini wa changamoto mbalimbali za kiusalama.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi