November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Ibuge ataka Mantra kushikirikiana
na TFS aina ya miti kupanda

Na Cresensia Kapinga ,Songea

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbart Ibuge ameitaka Kampuni ya uchimbaji wa Madini aina ya URANIUM yaliyopo Mto Mkuju Wilayani Namtumbo(MANTRA) kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Nchini (TFS) ili wawashauri kuhusiana na miti inayofaa kupandwa kulingana na eneo husika.

Wito huo umetolewa jana wakati alipotembelea banda la Kampuni ya Mantra, pamoja na banda la TFS wakati wa ufunguzi wa wiki ya Maadhimisho ya Kumbukizi ya Vita vya Majimaji.

Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka kuanzia Februari 23 hadi Februari 27, ambapo yanafanyika kwenye viwanja vya makumbusho hayo.

Ibuge amesema Serikali ipo kwenye mpango wa nchi nzima ya kupanda miti kitaifa, angalau milioni 1.5 kwa mwaka, hivyo wataondoka kwenye upandaji miti kizamani na badala yake kila mtu apande miti inavyostahili.

“Mtazamo wa Serikali kwa sasa ni kupanda miti kitaalamu ili kupunguza hewa ya ukaa kwa sababu ni ajenda ya kitaifa na ili tuwe na upandaji endelevu wa miti, hiyo kwa lengo la kutunza mazingira na vyanzo vya maji ni lazima TFS wahusike ili kushauri aina ya miti inayofaa kupandwa kulingana na eneo husika,” amesema Ibuge

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Generali Balozi Wilbert Ibuge akipata maelezo ya shughuli za Kampuni ya Mantra ambayo yalitolewa na Afisa Mahusiano wa kampuni hiyo, Adija Palangyo alipotembelea banda hilo kwenye maonesho ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Kumbukizi ya Vita vya Majimaji yaliyofanyika katika viwanja vya makumbusho ya majimaji yaliyopo Manispaa ya Songea leo.

Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa Ibuge kwenye banda la kampuni ya Mantra Afisa Uhusiano wa Kampuni hiyo, Khadija Palangyo alisema kuwa kampuni imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo upandaji wa miti kwa kushirikiana na idara ya mazingira (NEMC) na kwamba maelekezo yote ambayo yalitolewa na Mkuu wa Mkoa aliyapokea na atayafikisha eneo husika ili yaweze kufanyiwa kazi.

Awali Meneja TFS Kanda ya Kusini, Manyisye Mpokigwa alimwambia Mkuu wa Mkoa kuwa Wakala inashughulika na uhifadhi wa misitu asilia pia inajihusisha na ufugaji wa nyuki ambao hauhathiri mazingira

Mpokigwa amesema idara ya misitu na nyuki inajihusisha zaidi na ufugaji wa nyuki kisasa na upatikanaji wa asali, ambapo idara ya misitu inajihusisha na shughuli za kila siku za kuendeleza misitu iliyohifadhiwa kitaifa na misitu ya kupandwa ambayo itakuwa kivutio cha utalii.

Naye Mhifadhi Mkuu Shamba la miti Sao Hill Lucas Sabida alisema kuwa tunawaelimisha wananchi namna ya upandaji wa miti kisasa na uhifadhi wa miti hiyo kwa lengo la utunzaji wa mazingira,vyanzo vya maji pamoja na kibiashara.