November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi sita Tabora wakamatwa na Polisi

Na Allan Ntana, Tabora

JUMLA ya watumishi sita wa Halmashauri ya Manispaa Tabora wamekamatwa na Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kutowasilisha benki mapato waliyokusanya kiasi cha sh milioni 25.5.

Agizo la kukamatwa watumishi hao limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini, Komanya Kitwala baada ya kumalizika kikao cha dharura kilichoitishwa na DC na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Bosco Ndunguru, Mhasibu Amran Mteta na baadhi ya watendaji hao, watumishi 4 walikamatwa papo hapo.

DC ameagiza Jeshi la Polisi kuwasaka kokote waliko watumishi wengine wawili ambao hawakufika katika kikao hicho wakiwemo vibarua watano wanaotuhumiwa kukusanya mapato kiasi cha sh. milioni 1.2 na kuingia nazo mitini.

Amefafanua kuwa watumishi hao wanakwamisha juhudi za maendeleo katika manispaa hiyo ndio maana aliagiza Ofisi ya Mkurugenzi kumletea orodha ya watumishi wote waliokusanya mapato hayo na kutoyawasilisha benki ili sheria ichukue mkondo wake.

Amesema mtumishi yeyote aliyepewa dhamana na Serikali anapaswa kutekeleza wajibu wake ipasavyo na sio kufanya ujanja ujanja kwenye mapato ya Serikali, huu sio wakati wa kubeba watumishi wazembe wanaotanguliza maslahi binafsi mbele.

‘Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli inafanya mambo makubwa sana kutokana na kazi nzuri ya ukusanyaji mapato, hatuwezi kukubali mtumishi wa Serikali akusanye mapato na kuingiza mfukoni mwake’, amesema.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa, Bosco Ndunguru amesema kuwa hatua ya kukabidhi majina hayo imetokana na maazimio ya kikao cha Kamati ya Fedha kilichoketi Mei 22, 2020 kujadili taarifa ya mapato na matumizi ya halmashauri hiyo.

Amesema baada ya kupitia nyaraka zote za mapato yaliyoingizwa benki, kamati ilijiridhisha pasipo shaka kuwa watumishi hao saba na vibarua watano hawakupeleka benki fedha zote walizokusanya, hivyo wakaazimia kuwasilishwa majina yao kwa DC.

Mhasibu wa Manispaa hiyo, Amrani Mteta alitaja orodha ya watumishi wanaotuhumiwa kutowasilisha mapato ya halmashauri benki kuwa ni Ofisa Kilimo-Richard Mkama (Sh. milioni 2.3), Mlinzi-Salumu Daud (sh. milioni 12.28) na Mtendaji wa kata -Abdallah Mgemwa (sh. milioni 2.6).

Wengine ni Mtendaji wa Mtaa-Savela Fimbo (251,200/-), Mtendaji wa Mtaa-Hamis Abdul (310,000/-), Ofisa Mifugo-Cornelius Masawe (milioni 7.5) na Mtendaji wa kata-Cesilia Ernest (21,000/-) ambaye ilielezwa kuwa amelipa kwa kuchelewa hivyo kutakiwa kupewa onyo.

Alitaja watumishi (vibarua) watano  wanaotuhumiwa kutowasilisha makusanyo yao kuwa ni Mohamed Seif (232,000/-), Said Mzelela (166,000/-), Janet Mwanakatwe (43,000/-), Salma Choga (621,900/-) na Mohamed Mfaume (9,000/-), amesema