Ni za wabunge viti maalum waliotangaza kuhama NCCR-Mageuzi, yajibu kuhusu unyanyasaji
Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimejibu mapigo ya tuhuma zilizotolewa na wabunge wake wa viti maalum, Joyce Sokombi na Susan Masele kisha kutangaza kujiondoa ndani ya chama hicho na kuhamia NCCR-Mageuzi baada ya bunge kumalizika.
Tuhuma za wabunge hao zilijibiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Mwenyekiti wa Kanda na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa wiki hii wakati akihojiwa katika kipindi cha Jicho Pembuzi kinachorushwa na redio Ebony FM ya mkoani humo.
Mchungaji Msigwa, alisema anasikitishwa na kauli ya wabunge hao na kwamba anajua kuna wengine wawili watatu watafuata. Tulikuwa tunajua mapema wakati wa uchaguzi mkuu wa chama chetu,” alisema Mchungaji Msigwa huku akijibu tuhuma moja baada ya nyingine zilizotolewa na wabunge hao.
Kutopewa vyeo
Akianza na tuhuma za wabunge hao kuhusu kutopewa nafasi za uongozi ndani ya Chama, Mchungaji Msigwa alisema kikatiba kuna nafasi za kugombea na nafasi za kuteuliwa na kwamba kuna nafasi haupewi mwanamke kwa sababu ya kuwa mwanamke.
Alitolea mfano mbunge wa Kawe, Halima Mdee akisema alikuwa mbunge wa viti maalum, lakini baadaye aligombea akashinda Uenyekiti wa BAWACHA Taifa.
“Kwa hiyo wanataka mtu apewe uenyekiti wa taifa wa BAWACHA sababu yeye ni mwanamke?”Alihoji Mchungaji Msigwa. Alifafanua kwamba kuna nafasi za viti maalum vya kuingia Kamati Kuu ambavyo lazima achaguliwe mwanamke, kuna viti lazima achaguliwe mtu mwenye ulemavu, kuna nafasi za Zanzibar, lakini kuna nafasi za kugombania ambazo lazima mgombea awe na sifa.
Mchungaji Msigwa alisema yeye aliingia kwenye Kamati Kuu kwa sababu aligombea kwenye kanda akashinda, hakuna mwanamke aliyegombea nafasi hiyo akapambana naye akashinda, kwa sababu wagombea wote walikuwa wanaume.
“Ester Matiko kule (Kanda ya Serengeti) alipambana na Heche (John) akashinda yeye, hawa (Joyce Sokombi na Susan Masele) ni watu wanaotaka kubebwa bebwa kwa sababu ni wanawake, nafasi za kugombea hauwezi kubebwa,” alisema Mchungaji Msigwa na kuongeza kwamba upendeleo upo, lakini hoja zao hazina msingi wowote.
Tuhuma za kunyanyaswa kingono
Kuhusu madai ya kunyanyaswa kingono, Mchungaji Msigwa alisema; “Huyu anayelalamika ni mwanamke tena mbunge ambaye tulitegemea awe anawasemea watu wengine, lakini sasa anatokea yeye na kuanza kulalamika.
Amekaa miaka mitano bungeni,leo anaona zimebakia siku chache Bunge kuvunjwa, amesema alikuwa akinyanyaswa, alikuwa akinyanyaswa kivipi! Je wananchi wanatakiwa kumwamini mtu kama huyo? Hawa ni watu waliotengenezwa,” alisema Mchungaji Msigwa.
Alisema hoja hiyo imetengenezwa makusudi ili watu waache kujadili hoja. Alisisitiza kwamba watu wa aina hiyo huwa wanatengenezwa uchaguzi ukikaribia akitolea mfano mwaka 2015 kwamba kulikuwa na mbunge wa CHADEMA (jina linahifadhiwa) alikuwa anawatukana.
Mbali ya mbunge huyo Mchungaji Msigwa aliwataja wabunge wanasiasa wengine waliokuwa na tabia hiyo mwaka 2015 akisema walifanya vurugu nyingi, lakini leo hii hawapo kwenye duru za kisiasa.
Mchungaji Msigwa alisema ana imani hata wabunge hao wa viti maalum nao watapotea kisiasa, kwani CHADEMA ndiyo iliwabeba.
“Mbunge anashindwa kusoma hata hati (taarifa) ambayo ameiandika na hawezi kuieleza halafu amesema ni mbunge…mbunge wa viti maalum analalamika kunyanyaswa kijinsia? Je kama analalamika kunyanyaswa kijinsia mbunge wa aina hiyo anaweza kusimama na kuwatetea wanaonyanyaswa barabarani?”Alihoji Mchungaji Msingwa.
Hoja ya kuwa wabunge wapiga makofi
Kuhusu hoja ya wabunge hao kwamba ndani ya wabunge wa chama hicho, kuna baadhi ya wabunge wanaonekana ni wapiga makofi na wengine ndiyo maarufu, Mchungaji Msigwa alisema hiyo ni kwa sababu hawajiongezi thamani.
“Wanadhani kwamba ukipewa nafasi ya kuzungumza unaeleweka. Wale wanaoonekana maarufu wanasoma, wanatafiti wakisimama wanajenga hoja hata wao wenyewe wanajikuta wanapiga makofi…sasa wao wanashinda kwenye mabaa usiku wanaamka asubuhi wana…halafu ukimwambia leo asubuhi kuchangia, anakimbia atapataje huo umaarufu?”Alihoji Mchungaji Msigwa na kuongeza;
“Hatuwezi kusema mambo mengi hayo ni ya ndani, lakini utakuta mbunge anapewa dakika 15 za kuchangia, lakini utasikia akisema dakika tano zinatosha…vitu vizuri havisukwi, vinahitaji kutengenezwa, kwa hiyo hayo ni matatizo yao wao wenyewe.”
Alisema hata kwenye mpira ukiona kocha anampanga mchezaji maana yake huyo mchezaji ana matokeo…haiwezekani wewe unakuwa mbunge kwa miaka mitano haujatoa mchango ambao jimbo lako au taifa likasema walau kuna mbunge mmoja ameongea.”
Alisema wabunge hao walikuwa wanatumiwa na chama kimoja (anakitaja jina) na kwamba wamekuwa wakienda Iringa ili kuwatoa wananchi kwenye mstari wakiwadanganya watu kwamba mbunge wa CHADEMA hatatangazwa.
Alikituhumu chama ambacho alidai kilikuwa kimekufa na sasa kinazunguka nchi nzima kwamba mbunge CHADEMA hata mmoja hatatangazwa isipokuwa wa hicho chama.
“Kwa hiyo hakuna tunachokishangaa na kinachoendelea hata Iringa tunajua wanaowasiliana nao,” alisema.
Madai ya mfumo dume
Kuhusu madai kwamba ndani ya CHADEMA kuna mfumo dume, Mchungaji Msigwa alisema na wao wenyewe ni matokeo ya CHADEMA ili washiriki kuinua wanawake.
“Wao wenyewe wameenda bungeni kupitia wanawake kwa ajili ya kuwainua, wao wenyewe wamepata upendeleo ndani ya chama, halafu leo wanageuka wamesema kuna mfumo dume ndani ya CHADEMA, ni watu ambao hawajielewi,” alisema.
Mchungaji Msigwa alisema kwa yaliyotokea kwa wabunge hao chama hakijashangaa, wengi wao hawawezi kufanya mikutano walishakata tamaa. Alitolea mfano mbunge mmoja ambaye hakuwa na gari la kutembelea wakitoka bungeni anaomba rifti, akienda jimboni kwake anazomewa maisha yake yamemgomea.
Msigwa alisema CHADEMA ni taasisi kubwa changamoto kama hizo huwa zinatokea na wapinzani wao wanafanya kila kitu kuhakikisha wanashindwa, lakini wao wana macho wanaona ukweli ulivyo.
 Kuhusu Mbowe
Mchungaji Msigwa, alielezea kushangazwa kwake na kila anayetoka anamtupia lawama mheshimiwa Mbowe (Freeman), lakini mambo mengine wanaongea na kuafikiana.
Hata hivyo alisema wengine wameamua kusalitiana wakaamua kukaidi maagizo ya chama wakatoka.
“Wale sio kosa kwa wao kutoka, una hiari kwamba nisaliti chama halafu nifukuzwe, kwa hiyo walikaidi maelekezo ya chama hakuna mtu anayesema tulilazimishana, tulijadiliana wote kwa pamoja na kuishia kidemokrasia kabisa…tukakubaliana wenyewe wakaamua kukaidi wakatoka, sasa walipotoka kuna…ambao nao walikuwa wanawasubiri.
Ni sawa na mbuzi akitoka kwenye zizi wakati wenzake wote wamekaa kwenye zizi , akienda huko atakutana na mafisi wanamsubiri kwa hiyo na wao (wabunge) wakakamatwa na wakaanza kulishwa maneno , sema hivi ili CHADEMA ibomoke, mtukane Mbowe, sema hakuna demokrasia…sema haya. Hatimaye wakatoka, kwa hiyo ni hiari yao,” alisema Mchungaji Msigwa na kuongeza;
“Na kila mtu akitoka amesema Mbowe…Mbowe…Mbowe! Mbowe ni nani? Kwa kifupi tumefanya maamuzi ya kidemokrasia na kwa bahati mbaya mheshimiwa Spika akatumia eneo lile kisiasa zaidi na hata mimi ningelipata ningelitumia, akawachanganya watu ambao wamekubali kuchanganywa.”amesema
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja