Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi amesema Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ni wa kimkakati na kipekee kwasababu unamfikia mlengwa moja kwa moja kwenye Kaya yake na kumuwezesha kuboresha maisha yake.
Ndejembi ameyasema hayo Mkoani Songwe wakati wa kikao kazi chake cha kuhimiza uwajibikaji kwa Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa TASAF Ndejembi amewasisitiza maafisa hao kubuni miradi mbalimbali kwa ajili ya walengwa wa TASAF ili miradi hiyo iwe na tija katika kuboresha maisha yao.
Ameongeza kuwa, lengo la Serikali kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini ni kuzinyanyua kimaisha Kaya maskini, hivyo amewataka maafisa kuratibu shughuli za TASAF kwa weledi mkubwa ili kuisaidia serikali kufikia lengo lake.
Kwa upande wake, Mratibu wa TASAF, Mkoa wa Songwe, Atusungukye Dzombe amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa maelekezo aliyowapatia na kuahidi kuwa atahakikisha wanayafanyia kazi ili kaya lengwa ziondokane na umaskini.
Naye, Mratibu wa TASAF Wilaya ya Mbozi, Agnes Mwansembo, amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuwapa maelekezo yatakayoboresha utendaji kazi katika uratibu wa utekelezaji wa mpango wa TASAF, na kuongeza kuwa katika wilaya yake wamehamasisha uanzishwaji wa vikundi vya ujasiriamali na tayari wamefikia hatua ya utengenezaji wa Katiba ambayo itawawezesha walengwa hao kunufaika pia na mikopo ya Halmashauri.
Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Songwe yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini.
More Stories
Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar
CCM kuhitimisha kampeni kwa kishindo
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha