Na WAMJW – Dar es Salaam
SERIKALI imetoa ripoti ya uchunguzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyoko ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binaadam (NIMR) jijini Dar es Salaam na kubaini mapungufu mbalimbali ya kiutendaji yaliyokuwepo katika maabara hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu ametaja mapungufu yaliyobainishwa na kamati hiyo kuwa moja kati ya mashine za kupima sampuli za COVID-19 ilikuwa na hitilafu bila uongozi wa maabara kuchukua hatua za kuifanyia matengenezo.
Taarifa hiyo pia imebaini kuwepo kwa upungufu katika mfumo wa kimuundo, kiutendaji na uendeshaji wa kitaaluma katika upimaji wa vipimo, uhakiki wa ubora wa majibu na udhaifu katika uhifadhi wa vipimo vya COVID-19.
Waziri Ummy amesema kamati hiyo pia imetaja kuwepo kwa upungufu wa wataalamu wenye sifa za mafunzo ya “Biotechnology & molecular Biology” katika sekta ya Afya ikiwemo katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii.
Kufuatia taarifa ya kamati ya uchunguzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kuhusu upimaji wa sampuli za ugonjwa wa COVID- 19, Wizara ya Afya imechukua hatua ya kuhamisha shughuli za upimaji wa COVID – 19 kutoka kwenye maabara iliyoko NIMR na kuanza kutumika kwa mashine nyingine za maabara mpya iliyopo Mabibo, Dar es salaam.
“Kuanzia sasa shughuli zote za upimaji wa maabara ya taifa ya afya ya jamii zitafanyika katika maabara mpya ya mabibo yenye vifaa vya kisasa vyenye ubora na uwezo wa kupima sampuli 1,800 ndani ya masaa 24” amesisitiza Waziri Ummy.
Amesema maabara iliyokuwa inatumika awali na kukutwa na mapungufu ilikuwa na uwezo wa kupima sampuli 300 kwa masaa 24 na ilianzishwa mwaka 1968 katika ofisi za Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binaadam (NIMR), mtaa wa Obama kati kati ya jiji la Dar es Salaam zitaendelea kupima magonjwa mengine.
“hivi sasa Upimaji wa Sampuli zote za COVID-19 umehamishiwa kwenye Maabara hii ya Mabibo, Dar es Salaam ambayo kuanzia sasa ndiyo itakuwa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii. Maabara hii ambayo ujenzi wake umekamilika mwezi huu ina miundombinu inayojitosheleza, mashine za kisasa zinazoweza kupima sampuli nyingi na kutoa majibu ya uhakika na kwa haraka” amesema Waziri Ummy.
Aidha, Wizara imeshaandaa wataalam zaidi wenye sifa na vigezo kwa ajili ya Maabara hiyo na imeanza kurekebisha mfumo wa utawala, utendaji na kitaaluma ndani ya Maabara ya Taifa.
Waziri Ummy Mwalimu aliunda Kamati ya wataalam iliyoanza kazi rasmi tarehe 6, Mei, 2020 ya kuchunguza mwenendo wa maabara ya taifa ya afya ya jamii ikiwa ni pamoja na kuangalia mfumo mzima wa ukusanyaji na upimaji wa sampuli za COVID – 19.
Kamati hiyo iliundwa kufuatia mashaka yaliyoelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli kuhusu usahihi wa vipimo vya COVID – 1.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ametoa mwongozo wa kusaidia jamii kushiriki katika ibada ya shukrani na sala ya Eid El Fitr kwa hali ya usalama ili kuepusha kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Prof. Makubi amewataka wananchi kuchukua tahadhari katika siku tatu ambazo nchi itaingia katika maombi maalum ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kupungua kwa maambukizi ya virusi ugonjwa wa Corona.
“ ni muhimu wananchi wakasherehekea salama kwa kuchukuwa tahadhari kwani ugonjwa huo bado upo” Amesisitiza Mganga Mkuu wa Serikali.
Katika kufanikisha uwepo wa mazingira salama wakati wa shukrani na sala ,Viongozi wa Mitaa, Viongozi wa Afya na uongozi wa maeneo yote ya Ibada na misikitini wanapaswa kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kunawia mikono, maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono kwa ajili ya usafi binafsi wa waumini wote katika maeneo ya kuingilia .
Aidha, Prof. Makubi ameshauri sehemu za kufanyia ibada ziwe na nafasi ya viti kupangwa zaidi ya mita moja kwa wale wanaokaa au kusimama na wananchi wote wanapokwenda kushiriki au kutembelea maeneo ya Ibada/Sala wanashauriwa watumie barakoa za vitambaa ambazo kwa sasa zipo kwa wingi na zinatengenezwa hapa nchini na wananchi wenyewe.
Amewataka wananchi kuepuka mikusanyiko na kuhakikisha wanakaa umbali usipoungua mita moja kati ya mtu na mtu wakati wote wa shukrani na wakati wa shukrani waendesha ibada/sala wawakumbushe wananchi mara kwa mara kuzingatia taratibu za kujikinga na maambukizi kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya
Mganga Mkuu wa Serikali amewakumbusha Wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma kuzingatia maagizo ya Serikali ya kutosimamisha abiria kwenye mabasi, na vilevile wahudumu wote wawe wamevaa barakoa za vitambaa.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja