Na Cresensia Kapinga Songea, TimesMajira,Online, Songea
WAZIRI wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mkoani Ruvuma, Dkt Damas Ndumbaro amewataka wakazi wa Jimbo hilo na maeneo mengine kuitumia Hifadhi ya Wanyamapori ya Ruhila(ZOO) kwa kufanyia shughuli za mikutano au sherehe ili kuitangaza hifadhi hiyo katika maeneo mbalimbali.
Dkt. Ndumbaro ametoa mwito huo wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa jimbo hilo waliohudhuria sherehe za mwaka mpya wa 2022 katika eneo la hifadhi hiyo ambayo inasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Katika sherehe hiyo wananchi walipata kitoweo cha nyama pori (nyati), ambapo Waziri amesema wakazi wa jimbo hilo wana kila sababu ya kujivunia hifadhi hiyo kwa kuwa ipo mjini Songea, jambo ambalo hata utalii wake hautumii gharama kubwa kufika katika eneo la hifadhi hiyo .
Licha ya kuwataka wakazi hao kuitangaza hifadhi hiyo kwa kwenda kufanyia vikao mbalimbali pamoja na sherehe, amesema Wizara imejipanga kuiboresha zaidi kwa kujenga uzio ambao umeshatengewa fedha sh. milioni 500.
Dkt. Ndumbaro ambaye akiwa jimboni alitembelea milima ya uhifadhi wa Misitu ya Matogoro kisha kuzungumza na mamia ya wakazi wa Jimbo hilo, amesema mikakati ya kuboresha hifadhi hiyo ni pamoja na kuongeza wanyama kama simba ,chuwi ,mamba na twiga ili watalii wakifika katika eneo hilo wasikose kuwaona wanyama hao.
Aidha Waziri alizungukia baadhi ya maeneo ambayo yemetegwa kwa ajili ya uwekezaji wa vitu mbalimbali, ambapo katika mizunguko hiyo alitumia usafiri wa baiskeli.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, Hamis Abdalah Ally aliwapongeza wafanyakazi wa TAWA kwa kazi kubwa wanayoifanya katika hifadhi hiyo hasa ya kuilinda miti ya asili.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho amempongeza Waziri Dkt. Ndumbaro kwa kutekeleza ilani ya CCM kikamilifu katika sekta ya Maliasili na Utalii jambo ambalo limefanya kuwaleta watalii wengi kwenye vivutio mbalimbali vya hapa Nchini.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini