November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Malima atoa maagizo kwa wakandarasi waliosaini mikataba 16 ya miradi ya maji

Na Hadija Bagasha TimesMajira Online, Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima amewataka wakandarasi waliosaini mikataba 16 ya miradi ya maji Mkoani Tanga yenye zaidi ya thamani ya bilioni 10 kuhakikisha wanaikamilisha ndani ya muda uliopangwa.

Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya uingiaji wa mikataba 16 ya miradi ya maji inayotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa katika Mkoa wa Tanga.

Malima amesema Mkoa huo hautamvumilia mkandarasi atakayefanya mchezo na miradi ya maendeleo Mkoani Tanga kwa kuwa miradi hiyo ni muhimu kwa jamii na kwa kufanya hivyo ni kuifanya serikali iliyopo madarakani kuchukiwa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Aidha Malima amesema hataki kusikia mradi ya maji iliyosainiwa inakwama badala yake wahakikisha inatekelezwa kwa wakati na yenye tija ili malengo na maoni ya Rais Samia Suluhu kuhakikisha wananchi wanaondokana na adha ya huduma ya maji inatimia.

Alisema kwamba hataki kusikia kwamba miradi hiyo imekwama kwa kuwa wakandarasi wamefika na kuingilia makubaliano hayo hivyo ni matarajio yake itakamilika kwa wakati ili matamanio ya Rais Samia Suluhu yaweze
kufikiwa.

Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Upendo Lugongo amesema miradi hiyo inatekelezwa ndani ya miezi 6 huku katibu tawala wa Mkoa huo Pili Mnyema akisema miradi hiyo imekuja kwa wakati jamii ikiwa na uhitaji nayo.

Mhandisi Lugongo amesema mikataba hiyo inajumuisha mikataba 8 ya fedha za mfuko wa maji

(NWF) na mkataba mmoja fedha za Payment by result (PbR), mikataba 7 kupitia fedha za IMF (Uviko 19) ambapo unajumuisha jumla ya vijiji (33),Korogwe vijiji(7), Handeni Kijiji (1),Pangani vijiji ( 4),Muheza Vijiji (3),Lushoto Vijiji (6),Mkinga Vijiji (7) na Kilindi Vijiji (5).

Aidha alisema kwa wilaya ya Pangani ipo mikataba mitatu inayojumuisha vijiji (4) vya Kwakibuyu,Mkalamo,Mikunguni,na Stahabu ambapo Jumla ya watu 14,624 watapatiwa huduma ya maji kupitia ujenzi wa matanki matatu yenye ujazo wa mita (135,100,135) mtandao wa mabomba km 42.066 na vituo vya kuchotea maji 42 mikataba yote itagharimu kiasi cha zaidi ya Bilioni 1.6.

Mikataba hiyo16 ya maji imeingiwa kwenye wilaya 7 za Mkoa wa Tanga ambazo ni Pangani,Korogwe,Lushoto,Handeni,Muheza Mkinga na Kilindi mikataba ambayo inahusisha vijiji 33 vyenye jumla ya watu elfu 9543 sawa na asilimia 3.9.