Judith Ferdinand, Mwanza
Asilimia 80 ya walio washiriki wa maonesho ya 21 ya wajasiriamali wadogo na kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi/Jua Kali ni wanawake huku vijana wakiwa ni zaidi ya asilimia 60.
Hali hiyo inazidhirishia serikali za nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa zinahitaji kuimarisha sekta ya ujasiriamali ili kutekeleza kwa vitendo adhima yao ya kutoa fursa ya ajira kwa kiwango kikubwa kupitia makundi hayo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Omar Said Shaaban wakati akifunga maonesho hayo yalioanza Desemba 2 hadi 12, uwaja wa Rock City Malls,ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt.Hussein Mwinyi,yaliyofanyika mkoani Mwanza.
Shaaban amesema,amepata fursa ya kutembelea mabanda ya wajasiriamali wa nchi mbalimbali wanachama walioshiriki katka maonesho hayo na amevutiwa sana na ubunifu mkubwa waliouonesha wa kuandaa na kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa kutumia malighafi zinazopatikana kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki.
“Nimevutiwa zaidi kuona kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wajasiriamali niliowatembelea ni wanawake na asilimia zaidi ya 60 ni vijana,hali hii inadhihirisha sana kwamba serikali zetu zinahitaji kuimarisha sekta ya ujasiriamali kutoa fursa ya ajira,” amesema Shabaan.
Pia amesema, mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta hiyo ya ujasiriamali ambapo ukilinganisha ubora wa bidhaa za wajasiriamali kwa miaka ya nyuma na ubora wa bidhaa aliouona katika maonesho hayo kuna mabadiliko makubwa.
“Kutokana na ubora wa bidhaa zenu,nina hakika sasa mnao uwezo wa kuuza kwa wingi bidhaa hizo hata nje ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini wajasiriamali msiridhike na kiwango cha mafanikio mlioyapata sasa, tafuteni fursa zaidi,mzitumie na kila siku mlenge kupata mafanikio zaidi,”amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Mwakilagi ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,amesema maonesho hayo yamekuwa muhimu kwa wanamwanza na yameleta mzunguko wa fedha katika Mkoa huo kiuchumi.
Amesema watu wameweza kununua vitu mbalimbali ambapo wageni wamekula vyakula pamoja na samaki watamu wanaopatikana katika mkoa huo.
Sanjari na hayo wageni wameweza kutembelea vivutio mbalimbalil vya utalii vilivyopo mkoani Mwanza ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya maonesho hayo ambapo kwa mwaka huu wajasiriamali wameweza kupata mabanda bure tofauti na awali walikuwa wanalipia hakika mkono wa mama ndio unao lea,”amesema Mwakilagi.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Wajasiriamali Jumuiya ya Afrika Mashariki Josephat Rweyemamu,amesema wajasiriamali hao wameuza na kutengeneza mtandao wa biashara nchini Tanzania na Kenya.
Hiyo imesababishwa na kuwa na sehemu salama na pazuri ambayo huchangia kutoa fursa kubwa ya kufanya biashara.
Rweyemamu amesema, wajasiriamali hao wameshukuru serikali zao na waneziomba ziendelee kuwasaidia ili waweze kuzunguka katika nchi za Afrika Mashariki.
Pia amesema, wajasiriamali hao wameandaa mpango wa kuuza bidhaa kwa njia ya mtandao.
“Kuanzia Januari,2022 tutaanza rasmi zoezi hilo la kuuza bidhaa kwa njia ya mtandao ambapo ukiwa Mwanza,Dar-es-Salaam, Zanzibar unaweza kuagiza bidhaa kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na bidhaa ikakufikia,”amesema Rweyemamu.
Aidha amewataka wajasiriamali hao kujiandaa kuwa na bidhaa nzuri kwa ajili ya maonesho hayo ya 22 yanayotarajiwa kufanyika mwakani nchi Uganda na zitakazoweza kuuzika katika soko SADC.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa