Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) Gerald Mweli amezitaka Kamati za Tume ya Utumishi wa Walimu kutoa mafunzo kwa walimu wapya ili kuwajengea uwezo kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
Pia ameziagiza kamati hizo kutoa mafunzo kwa walimu ambao wanaonekana kukiuka maadili ya taaluma hiyo na kufanya makosa ya mara kwa mara ili warudi kwenye mstari na kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Akizungumza na Kamati hizo kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Magharibi Mweli amesema,mafunzo hayo yatasaidia makundi hayo kufanya kazi yao kwa kufuata miongozo,sheria na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya kada hiyo ya ualimu.
“Mafunzo haya mnayoyapata na ninyi mkayatoe kwa walimu wapya huko katika maeneo yenu ,lakini pia wapo walimu ambao walishapewa mafunzo lakini bado wamekuwa wakifanya makosa ya kujirudia rudia,nao nendeni mkawaite na kuwapa mafunzo badala ya kukimbilia kuwapa adhabu .”amesema Mweli na kuongeza kuwa
Aidha amesema kamati hizo zimepewa jukumu la kufuatilia maadili ya walimu huku akisema wanapaswa kuliangalia suala hilo kwa umakini mkubwa na kutoa adhabu inayomstahili mwalimu kulingana na kosa alilolitenda.
“Mkumbuke mmepewa jukumu na mustakabali wa ajira za walimu upo mikononi mwenu,maamuzi mnayoyafanya ni ya kutazamwa na kuyafanya kwa kutenda haki ,kwenye kosa mwalimu apewe adhabu anayostahili lakini msisubiri watu wafanye makosa ili wawaadhibu,
“Muwajengee walimu wapya uwezo ,pia na walimu ambao hawaendi sawasawa muwape mafunzo ,maana Serikali haipendi mwalimu afukuzwe kazi maana unakuta wengine tayari wana uzoefu wa miaka kumi,kwa hiyo tunapenda wabaki shuleni .”amesema Mweli
Mweri amezitaka kamati hizo kuhakikisha chombo hicho kinakuwa baraka katika kutatua na kupunguza changamoto za walimu badala ya chombo hicho kugeuka laana .
Amesema,kwa upande wa Tamisemi ,itaendelea kushirikiana na TSC katika kuhakikisha mnapata vitendea kazi .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Profesa Willy Komba aMEsema mafunzo hayo yatawawezesha watendaji hao kusimamia sheria kanuni na taratibu kama zilivyowekwa katika ajira zao.
“Tume hii imeamua kuendelea kuwapatia watendaji mafunzo ili wajitambue wao ni wakina nani na si kuwaacha wafanye makosa ndipo waadhibiwe au kufukuzwa kazi,ukishamfukuza mwalimu kutafuta pengo lingine la kuziba ni kazi, hivyo tutaendelea kutoa mafunzo haya kwa awamu kutokana na upatikanaji wa fedha” amesema Profesa Komba
Aidha amesema,tangu waanze kuwawezesha watendaji hao wa kamati za wilaya malalamiko yamepungua kwa kiasi kikubwa na tayari wameshazifikia kanda tano kwaajili ya utoaji mafunzo hayo.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi