Na Martha Fatael,TimesMajira Online, Same
WATUMISHI wa umma hususani viongozi wa serikali za mitaa mkoani Kilimanjaro wameonywa kuacha mara moja kutumika kama daraja la kupitishia fedha zisizohalali katika akaunti zao za benki kwani watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) mkoani hapa imesema inafuatilia kwa karibu mienendo ya baadhi ya watendaji hivyo imewataka kuwa makini na fedha zinazopitishwa kwenye akaunti zao badala ya kuzichukua na kuzitumia kwenye shughuli zao binafsi.
Kauli hiyo imetolwa na Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Frida Wekesi wakati anawasilisha mada Katika semina hiyo iliyohusisha viongozi wa vijiji na kata katika Jimbo la Same Magharibi kuhusu umuhimu wa uaminifu na athari za rushwa kwa viongozi wa serikali za mitaa pamoja na Chama Cha Mapinduzi ngazi za shina na kata.
Amesema makosa ya kutumiwa fedha zisizojulikana chanzo halali cha mapato yake na kuzitumia katika shughuli halali yanaangukia katika makosa ya utakatishaji fedha ambayo haya dhamana hivyo watapoteza kazi zao.
“Usifikiri unapotumiwa fedha zisizohalali na kuzitumia kujenga nyumba, kununua vitu vya thamani yakiwemo magari, kulipa ada za watoto shule kunaleta uhalali wa zile fedha la hasha!….ikitokea ukafanya hivyo ni kiknyuma na sheria, epukeni huo mtego”amesema Wekesi.
Wekesi amesema fedha zozote zinazotumwa kwenye akanti za fedha zinapaswa kuwa na maelezo ya kutosheleza ikiwemo ushahidi wa maelezo hayo kwani zitakapobainika kutokuwa halali utaunganishwa katika makosa ya utakatishaji fedha mpaka itakapothibitika vinginevyo.
“Kutokujua sheria sio kinga….mnapaswa kujiridhisha na fedha zote zinazotumwa kwenu kabla ya kuzitumia maana tukikukamata na rushwa ama utakatishaji fedha hatutaangalia kama wewe ni kiongozi, mtumishi mwenzetu ama la, tutaangalia kama unahusika kwenye kosa tu”amesema
Aidha Kamanda Wekesi pia ametaka viongozi hao kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutochagua viongozi wa ngazi mbalimbali kwa misingi ya rushwa kwani hawatapata maendeleo.
Akizungumza katika mafunzo hayo, afisa uhamiaji mkoani Kilimanjaro, Martin Mwenda ametaka viongozi wa ngazi mbalimbali kufanya utambuzi wa wageni wote wanaohamia katika maeneo yao kwani kazi kubwa ya kwanza ni ulinzi katika makazi.
“Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa iliyopo mipakani mwa Tanzania na nchi nyingine hivyo ni vyema jukumu la kwanza la viongozi wote kuhakikisha hatuwi daraja la wahamiaji haramu”amesema.
Mafunzo hayo yanayotegemewa kufanyika katika majimbo yote Tisa ya mkoa wa Kilimanjaro yameandaliwa na serikali mkoani hapa kwa kushirikiana na CCM ili kujenga uelewa wa pamoja baina ya viongozi wa serikali na wa CCM na kuepuka misuguano isiyo ya lazima.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea