Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dar
WAJUMBE mbalimbali wa Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) wameeleza mikakati yao katika kueneza elimu ya usuluhishi wa migogoro na amani katika nchi zao mara baada ya kupokea mafunzo ya siku tatu juu ya usuluhishi wa migogoro katika ngazi ya jamii.
Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa semina hiyo ya mafunzo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, wajumbe hao wameeleza kufurahishwa na mafunzo na kwamba yamewaongezea maarifa ambayo watakwenda kutumia katika nchi zao kwenye kusuluhisha migogoro.
Mjumbe na mshiriki wa mafunzo hayo kutoka nchini Zambia, Brigedia Jenerali Joyce Ng`wane Puta ameishukuru Interpeace kwa kuja na mpango mzuri wa kuwapa elimu ya amani na usuluhishaji wa migogoro washiriki wote kutoka nchi za maziwa makuu, huku akiamini kuwa jambo hilo litachochoe uwepo wa amani kwenye mataifa wanayotoka hivyo mpango huo utakuwa na tija kwa ustawi wa mataifa hayo.
“Tumefundishwa kutoa suluhisho la migogoro na amani kwa kuanzia ngazi ya chini kabisa kwenye jamii zetu kitu ambacho kwangu ninakiona ni kizuri kwa kuwa tukipandikiza amani kwenye ngazi ya familia itakuwa rahisi hata kwa vizazi vijavyo kukuta mfumo huu ambao utazifanya nchi zetu kuwa sehemu salama kwa maendeleo,” amesema Brigedia Jenerali Puta.
Ameongeza kuwa yeye kama mshiriki na mnufaika wa mafunzo atatumia ujuzi alioupata kwenda kuboresha mahusiano mazuri kwao, “Ninajivunia sana kupata mafunzo haya na elimu hii nitaitumia kama fursa kwangu kwenda kuwa balozi kwenye jamii yangu ninayotoka kuhakikisha kuwa ninakuwa mstari wa mbele kuchochea amani na kusuluhisha migogoro kwenye jamii”.
Naye Anastase Nabahire ameelezea furaha yake baada ya kumaliza mafunzo hayo, huku akibainisha faida kubwa ya mafunzo hayo kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha watu pamoja kama moja ya matokeo ya uwepo wa amani ya kwenye taifa lolote lile.
“Amani siku zote inazaa umoja, na sisi kama wa Afrika tuna nafasi kubwa ya kuungana pamoja kama mataia yote endapo tutakuwa na amani, hivyo basi hiki nilichojifunza kitakwenda kuboresha kwenye jamii yangu pale ambapo pamekuwa na machafuko na kupelekea kuhatarisha amani,” amesema Nabahire.
Ameongeza kuwa, “Uwepo wa mafunzo haya unasaidia sana kwa ustawi wa mataifa yetu ukanda wa maziwa makuu na binafsi nimefarijika sana kuwa moja wa nufaika wa mafunzo haya”.
Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo Dkt. Agge`e Shyaka Mugabe mbali ya kuwa na imani kubwa kwa washiriki wa mafunzo hayo, amesema mafunzo hayo yaliyoshirikisha nchi 12 yalijikita katika kuwajengea uwezo wa usulihishaji wa migogoro na amani washiriki kutoka mataifa hayo yaliyo kwenye ukanda wa maziwa makuu.
“Matarajio yangu ni makubwa kwa kuwa tuna timu mzuri ya washiriki, na nina imani kubwa kile walichokipata kitakwenda kuwa na manufaa makubwa ya kuzifanya jamii zetu kwenye ukanda wetu kuwa jamii salama zenye amani na utulivu”, amesema Dkt. Mugabe.
Aidha Dkt. Mugabe amebainisha kuwa kwa kuwa sehemu kubwa ya washiriki kwenye mafunzo hayo ni wananwake na vijana, jambo ambalo amesema ni sehemu kubwa ya watu wenye ushawishi mkubwa kwenye jamii hivyo itakuwa kazi rahisi kwao kuwafikia na kuwapa elimu watu wanaowazunguka.
“Wanawake na Vijana ni makundi yenye ushawishi mkubwa kwenye jamii na hata sisi hapa kwenye mafunzo yetu tuna akina mama na vijana wengi tu, hii inatupa picha kuwa washiriki hawa wataenda kuyafikisha haya waliyojifunza kwa urahisi kwenye maeneo wanayotoka”.
Mafunzo yaliyofungwa jana haya yanatarajiwa na mataifa ya ukanda wa maziwa makuu kuwa chachu ya usluhishaji wa migogoro na amani kwenye jamii huku pia matarajio hayo yakiwa kuzifanya nchi hizi kuwa sehemu imara ili kuzifanya kuwa sehamu salama kwa maendeleo ya watu wake.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini