Na Martha Fatael, Moshi,timesmajira
SERIKALI imeahidi kuwekeza kwenye tafiti za kina kutafuta sababu za kuongezeka kwa udumavu kwenye mikoa inayoongoza kwa uzalisha mkubwa wa vyakula vinavyotakiwa kwenye ukuaji wa watoto.
Aidha taasisi za utafiti wa mazao nchini zimetakiwa kuongeza jitihada katika kuhamasisha kilimo cha mbegu bora na kwa njia za asili ili kuongeza ufanisi na lishe bora kwa rika zote.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai amesema hayo wakati akizindua siku ya chakula Duniani inayofanyika kitaifa mkoani Kilimanjaro katika viwanja vya Shule ya msingi Mandela mjini hapa.
Amesema serikali kupitia taasisi zake za utafiti nchini na kwa kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa itaongeza nguvu katika tafiti mbalimbali lakini pia katika utafiti huu wa kutafuta sababu za ongezeko la udumavu kwenye mikoa yenye uzalishaji mzuri wa vyakula.
“Tuna hali nzuri sana ya uzalishaji wa chakula hapa nchini kiasi cha kwamba tumeruhusu uuzaji wa mazao nje ya nchi….lakini ni muhimu kuwakumbusha tunapaswa kuhifadhi vyakula kwa ajili ya matumizi yetu kama miongozo inavyosema”alisema
Mkuu wa mkoa huyo amesema mahitaji ya chakula nchini kwa mwaka 2021/22 ni Tani 14,796,751 ikiwa ni ziada ya Tani 3,628496 hivyo hakuna athari iwapo watanzania watauza mazao yao kwa masoko ya ndani na nje ya nchi.
Awali naibu waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel ametaja mikoa inayoongoza kwa udumavu nchini kuwa ni Songwe, Mbeya, Iringa na Ruvuma na kwamba ipo haja ya kutafuta sababu za Udumavu licha ya kuongoza kwa uzalishaji wa chakula.
Naibu waziri huyo ametaka Mamlaka nyingine ikiwamo ya TFDA, kuwasaidia wakulima wanaoongeza thamani ya mazao yao ili wapate vibali mapema badala ya kuchukua muda mrefu na kupata hasara.
Akiongea katika maadhimisho hayo,Mkuu wa program ya usambazaji tecknolojia na mafunzo Dr. Jeremiah Magesa kutoka taasisi ya utafiti wa zao la kahawa nchini(TaCRI), amesema taasisi hiyo inashirikiana na taasisi nyingine katika kuhamasisha matumizi ya mbegu bora za kahawa katika kupanua wigo wa uzalishaji wa kahawa.
Amesema kwa kushirkiana na bodi ya kahawa mwaka huu imezindua mpango mkakati wa miaka mitano wa kuzalisha miche Milioni 20,000 ifikapo 2025/26 ili uzalishaji wa kahawa Tanzania ufikie tani 300,000 kutoka tani 68,000 kwa mwaka kupitia aina mpya ya mbegu ya kahawa ya chotara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwaka Jana katika maadhimisho kama hayo, ilibainishwa kuwa mkoa wa Njombe ulikuwa na udumavu wa asilimia 53.6 wakati uzalishaji mazao ni tani 446,49, ikifuatiwa na mkoa wa Rukwa ulikua na udumavu wa asilimia 47.9, huku uzalishaji ni tani 943,002 na kiwango cha Utoshelevu-SSR asilimia 230.
Huku Iringa ilikuwa na udumavu wa asilimia 47.1, huku uzalishaji ni tani 470,750 na kiwango cha utoshelevu-SSR asilimia 161 ikifuatiwa na Songwe ilikuwa na udumavu asilimia 43.3 huku uzalishaji mazao ni tani 805,545 na kiwango cha utoshelevu cha asilimia 210.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito