November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali Zanzibar yataka mawasiliano kufika sehemu zote za muungano

Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

WAZIRI wa Mawasiliano na Uchukuzi  wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Rahma Kassim Ali ametembelea Ofisi za Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) zilizopo katika chuo kikuu Dodoma na kuutaka  mfuko huo kuongeza juhudi zaidi za kufikisha mawasiliano katika sehemu zilizo na changamoto za Mawasiliano pande zote za Muungano ,Zanzibar na Tanzania bara

Akizungumza mara baada ya kuwasili katika ofisi hizo Waziri huyo wa Mawasiliano na Uchukuzi serikali ya Mapinduzi Zanzibar,  

Amepongeza juhudi zinazofanywa na  Mfuko huo katika kuhakikisha mifumo ya Mawasiliano inamfikia kila Mtanzania.

“Ni vyema mkaongeza juhudi katika kutatua changamoto za mawasiliano hasa katika maeneo ambayo yanachangamoto izo kwa bara na Zanzibar hasa katika maeneo ya vijijini,kuna baadhi ya maeneo tunakokwenda kufanya kazi tunakutana na changamoto za kutokuwepo kwa mtandao hili mkalifanyie kazi kwa kushirikiana na kuhakikisha mnamaliza,”amesema.

Naibu Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa katika kujibu mahitaji ya watanzania kwenye suala mawasiliano utafiti ni jambo la Msingi.

“Nyie kama mfuko wa mawaailiano kwa wote mnatakiwa kuhakikisha mnafanya utafiti kwanza kabla ya kuenda kupeleka minara sio kunipeleka tu na kuiacha ni muhimu kujua mmepeleka mingapi na kuisimamia kwa kufanya utafiti wa eneo husika,”amesema Naibu waziri.

Mtendaji mkuu wa Mfuko wa mawasiliano kwa Wote Justina Mashiba  ameanisha miradi wanayotekeleza ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo cha miito ya simu za dharura Zanzibar na mpango wa kuunganisha shule kwenye mtandao wa internet ili kurahisisha wanafunzi kujisomea.

“Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF),hadi kufikia Septemba mwaka huu umesaini mikataba 41 ya miradi ya kupeleka mawasiliano vijijini katika kata 1,068 ambazo zina vijiji 3,279,”amesema.

Amesema Kuwa Miradi hiyo ikikamilika itafikisha huduma za mawasiliano ya simu kwa watanzania Milioni 12.8,Aidha,aliema kwa upande wa Zanzibar,Unguja na Pemba kuna miradi katika Kata 12 na ikikamilika itawasaidia watanzania  41,440 kutapata huduma za mawasiliano.

Kwa upande wake Waziri  Uchukuzi na Mawasiliano Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alitembelea katika mradi wa ujenzi wa ofisi mpya Mfuko wa Mawasiliano kwa wote unaogharimu Tsh.Bilioni 2 ambapo hadi sasa umefikia asilimia 65  ukiwa unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu na jumla ya Tsh.milioni 900 zikiwa zimeshatumika .