November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dc Mbeya asema Rais Samia atambua umuhimu wa wakulima

Na Esther Macha,Timesmajira,Online, Mbeya

SERIKALI  Mkoani Mbeya imesema kuwa  Rais wa Jamhuri wa muungano wa Tanzania Rais ,Samia Suluhu Hassan  kwa kutambua umuhimu  wa wakulima ameendelea kulinda  na kutetea maslahi ya wakulima Tanzania  kwa kuwa na  vikundi  kadhaa  vinavyosaidia wakulima pamoja na taasisi za kifedha  za ndani na  nje ya nchi.

Imeleezwa kuwa kuwepo kwa taasisi hizo ni usimamizi imara wa serikali hivyo Rais Samia Suluhu Hassan anapaswa kupongezwa kwa kazi kubwa anayofanya  chini ya serikali yake ya awamu ya sita.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa  maduka ya pembejeo za kilimo za Kampuni inayotoa huduma  za kilimo na pembejeo(One Acre Tanzania),Mkuu wa  wilaya ya Mbeya ,Rashid  Chuachua ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya  amesema  kwamba  zipo benki nyingi ambazo zimekuwa zikijikita kukopesha pembejeo kwa wakulima  pamoja na kupata huduma za kifedha ili kupata tija kwenye mazao yao.

“Lakini pia tunayo mashirika kama One Acre  Tanzania wao wanaweza kukopesha pembejeo au kuwauzia wakulima kwa gharama wanayomudu ili kupata tija katika mazao yao ,sambasamba na hiyo kampuni hiyo inawekeza teknolojia ya kisasa ya kupata habari na kupata huduma za kilimo  kwa ajili ya kuboresha tija kwenye sekta ya kilimo nchini”amesema Mkuu huyo wa Wilaya.

Akielezea zaidi Chuachua alisema serikali imeendelea kutoa maelekezo kadhaa kwa halmashauri zote nchini kwa ajili ya kuimarisha sekta ya kilimo ambapo kwa mwaka huu wa feha halmashauri ya wilaya imetenga Bil.178 kwa ajili ya kuimarisha sekta hiyo .

“Lakini pia nimepata taarifa kuwa Wilaya ya chunya imetenga Bil.140, wakati  katika kuimarisha mahusiano  na kwamba serikali imekaribisha wahisani wa serikali ya marekani ambapo wametoa fedha Bil.260 kwa shirika la agree Konet  ambapo wanatoa huduma mbali mbali  za kilimo, barabara,na  hata barabara ya inayotoka  Inyala kwenda Simambwe imejengwa kwa ajili kutoa huduma kwa wakulima ”amesema  Mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Mbeya.

Aidha Chuachua amesema  amefurahishwa na kitendo cha kampuni hiyo kuzidi kuwekeza kwenye tafiti na teknolojia  ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wakulima ambapo walianza  na vijiji vitatu vyenye wakulima  433 mwaka 2016 na sasa wameweza kuwafikia wakulima 6,957 kwenye vijiji, 37 kwenye msimu wa 2021 na kwamba hiyo inaaminisha kuwa wakulima wameendelea kuona tija zinazotolewa na kampuni hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wilaya ya Chunya ,Saimon Mayeka amewataka wakulima kutembea kifua mbele kutokana  na jitihada wanazofanya za kuhakikisha chakula kinakuwepo mjini bila wakulima kupeleka shibe hakuna kitachoendelea .

Kwa upande wake ofisa uhusiano wa kampuni inayotoa huduma za kilimo na pembejeo(One Acre Tanzania limited )Dorcas Tinga amesema  kuwa   maduka yaliyofunguliwa kwa kampuni hiyo ni 16 mkoani Njombe  na kwamba kwa mikoa ya  Mbeya na Songwe wamezindua maduka 12 ambapo kati ya hayo  maduka 9 yapo Mbeya na matatu Songwe  huku akisema muundo huu mpya utawezesha wakulima kupata pembejeo zenye ubora mwaka mzima.

Aidha Tinga alisema ilianzishwa mwaka 2013 na kuwa mpaka sasa inahudumia wakulima 60,000 na kwamba kampuni hiyo inafanya kazi na mikoa mitano ambayo ni , Iringa,Songwe,Mbeya na Arusha  kwa kuwapatia wakulima wadogo ufahili  na mafunzo wanayohitaji ili kujiwekea njia za kudumu za kufanikiwa.

Hata hivyo Tinga amesema  kuwa pia katika mafunzo wanayotoa wanafundisha  njia ambazo zitawapelekea kuvuna kwa tija, na namna ya kuongeza kipato kupitia mazao yao  na kwamba kwasasa Kampuni ya one acre Tanzania inahudumia wakulima mil.1 nchini Kenya ,Rwana,Burundi,Tanzania,Uganda,Zambia pamoja Malawi.

Mmoja wa wakulima wa kijiji cha Imezu wilaya ya Mbeya  ,Telezia Mponzi amesema anashukuru uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kuwajali wakulima wa hali za chini  ambao hivi kilimo kimekuwa neema kwao  na kufakiwa kusaidia familia zao kusomesha na kukidhi mahitaji mengine muhimu ya kifamilia.