Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
WIZARA ya Kilimo imesema kuwa, Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani mwaka huu hapa nchini yatafanyika Kitaifa mkoani Kilimanjaro.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Kilimo,Prof. Adolf F. Mkenda huku akisisitiza kuwa, yatafanyika Oktoba 10 hadi 16,mwaka huu.
“Ndugu wananchi, tarehe 16 Oktoba ya kila mwaka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huungana na nchi wanachama wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika kuadhimisha Siku ya Chakula Duniani.
“Chimbuko la maadhimisho haya ni Mkutano wa mwaka 1979 ambapo Nchi Wanachama wa FAO walikutana jijini Quebec nchini Kanada na kujadili masuala mbalimbali kuhusu chakula. Mojawapo ya maazimio ya mkutano huo ilikuwa kufanya Maadhimisho ya Siku ya Chakula kila mwaka ili kutathimini na kuweka mikakati ya upatikanaji wa chakula cha kutosha, salama na chenye virutubishi kwa watu wote na kwa wakati wote.
“Maadhimisho ya kwanza ya siku ya Siku ya Chakula duniniani yalifanyika mwaka 1981. Hivyo maadhimisho ya mwaka huu ni ya 41, na yanasherehekewa sambamba na wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN General Secretary) alioutoa mwaka huu, kuzitaka nchi wanachama kutathmini na kuboresha mifumo yake ya chakula, ili kuchochea kasi ya kufikia Malengo 17 ya Dunia ya Maendeleo Endelelevu,”amebainisha Waziri wa Kilimo, Profesa Mkenda.
Profesa Mkenda amefafanua kuwa, kila mwaka Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) huchagua kauli mbiu ambayo huwa inatoa dira ya kuhamasisha wadau wote wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuchangia katika kuhakikisha kila mtu anawezeshwa kupata chakula bora na cha kutosha wakati wote wa maisha yake. Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema Zingatia Uzalishaji na Mazingira Endelevu kwa Lishe na Maisha Bora
“Kwa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na mikoa jirani nawaomba mjitokeze kwa wingi kwenye maadhimisho haya ambayo yatazinduliwa rasmi kitaifa tarehe 10 Oktoba, 2021 na kufikia kilele chake tarehe 16 Oktoba, 2021 katika viwanja vya shule ya msingi Pasua, Manispaa ya Moshi-Kilimanjaro.
“Ndugu wananchi,Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kutekeleza kauli mbiu hii kwa kuhakikisha uzalishaji wa chakula nchini unaimarika na kutosheleza mahitaji ya nchi kwa kipindi chote. Hali ya chakula mwaka huu imeendelea kuwa nzuri kutokana na uzalishaji mzuri katika msimu wa 2020/2021.
“Tathmini iliyofanyika hivi karibuni imeonesha kuwa hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa na kimkoa katika msimu wa 2020/2021 na upatikanaji wake kwa mwaka 2021/2022 umefikia tani 18,425,250 kwa mlinganisho wa nafaka (Grain Equivalent) ambapo nafaka ni tani 10,869, 596 na yasiyo nafaka tani 7,327,137. Ikilinganishwa na msimu wa 2019/2020 ambapo uzalishaji ulikuwa tani 18,196,733, kumekuwa na ongezeko la uzalishaji wa tani 1,903,096 ambalo ni sawa na asilimia 10.5. Uzalishaji wa mahindi unatarajiwa kufikia kiasi cha tani 6,908,318 na mchele kufikia kiasi cha tani 2,629,519,”amefafanua Waziri Mkenda.
Mheshimiwa Waziri amebainisha kuwa, mahitaji ya chakula kwa 2021/2022 nchini, ni tani 14,796,751, ikilinganishwa na uzalishaji, nchi inatarajiwa kuwa na ziada ya tani 3,628,499 za chakula ambapo tani 1,222,103 ni za mazao ya nafaka na tani 2,406,396 ni za mazao yasiyo nafaka. Kiwango hiki cha uzalishaji kitaiwezesha nchi kujitosheleza mahitaji yake ya chakula kwa uwiano wa utoshelevu ( Self Sufficient Ratio-SSR ) wa asilimia 125.
Profesa Mkenda ameendelea kubainisha kuwa, pamoja na nchi kutarajiwa kuwa na utoshelevu wa chakula kwa kiwango cha Ziada (SSR ya 125), bado kuna Halmashauri 17 katika Mikoa 8 zenye maeneo yenye dalili za upungufu wa chakula kwa mwaka 2021/2022.
“Hali hii ni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mtawanyiko mbaya wa mvua na visumbufu vya mazao shambani vilivyojitokeza katika msimu wa uzalishaji 2020/2021. Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama wa chakula katika maeneo hayo ili kuhakikisha hali ya utengamano inaendelea kuwepo.
“Hali ya lishe nchini si ya kuridhisha kutokana na takwimu kuonesha viwango vya juu ya utapiamlo hasa katika mikoa inayoalisha vyakula kwa wingi. Serikali imeendelea na juhudi za kuhakikisha hali ya utapiamlo nchini inapungua kupitia mikakati na programu za kitaifa zinazoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara za Kisekta na Wadau wa Maendeleo.
“Takwimu zinaonyesha udumavu umepungua kutoka asilimia 34.7 mwaka 2014 hadi asilimia 31.8. Pamoja na mafanikio haya bado idadi ya watoto wenye udumavu ni zaidi ya milioni tatu, hali ambayo haikubaliki ikikilinganishwa na kiwango cha asilimia 28 ya udumavu kilicholengwa kufikiwa kitaifa,”ameeleza Waziri.
Kwa upande wa hali ya ukondefu,Mheshimiwa Waziri Mkenda ameeleza kuwa, lengo lilikuwa ni kupunguza hadi chini ya asilimia 5. Ukondefu umepungua kutoka asilimia 3.8 mwaka 2014 hadi asilimia 3.5.
“Aidha, bado tunakabiliwa na utapiamlo unaotokana na ukosefu/upungufu wa virutubishi mwilini ambavyo ni Vitamini na Madini kama vile madini chuma, madini joto (Iodine) na zinki.
“Ndugu wananchi,takwimu zinaonesha kuwa Mikoa inayozalisha chakula kwa wingi ndiyo yenye viwango vya juu vya udumavu kwa watoto mfano, Njombe asilimia 53.6, Rukwa asilimia 47.9, Iringa asilimia 47.1, Songwe asilimia 43.3, Kigoma asilimia 42.3 na Ruvuma asilimia 41.0.
Kwa upande wa Nyanda za juu Kaskazini mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, viwango vya udumavu si vya kuridhisha ingawa viko chini ikilinganishwa na mikoa tajwa hapo juu. Takwimu zinaonesha kuwa hali ya udumavu kwa mkoa Kilimanjaro ni asilimia 20.0, Arusha 25.2, Manyara 36.1,”ameongeza Waziri Profesa Mkenda.
Aidha, Waziri wa Kilimo amesema kuwa, Mkoa wa Kilimanjaro una changamoto ya tatizo la lishe iliyozidi (uzito uliozidi au kiribatumbo) kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa (miaka 15 49) ambayo imefikia asilimi 49.0.
“Kiwango hiki kiko juu ikilinganishwa na wastani wa kitaifa ambao ni asilimia 31.7, kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu duni ya matumizi ya chakula na lishe kwa watanzania walio wengi.Ndugu wananchi,Madhumuni ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ni kuendelea,
“Kutoa elimu kwa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kwa kujifunza mbinu na teknolojia sahihi za kuongeza uzalishaji wenye tija na endelevu katika Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kupata chakula bora na cha kutosha kwa kila mtu na kwa wakati wote;
Kuelimisha na kuhamasisha na wananchi kutumia vyakula vya asili vyenye virutubishi kwa wingi na kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara; Kuhamasisha matumizi ya mbegu za asili na kilimo chenye kuhifadhi mazingira;
Kutoa elimu ya umuhimu wa mila na utamaduni katika kuendeleza sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji ili kuboresha hali ya usalama wa chakula na lishe,”amesisitiza Waziri Mkenda.
Kwa mujibu wa Waziri Profesa Mkenda, wakati wa maadhimisho hayo; shughuli zifuatazo zitafanyika ili kufikia malengo na madhumuni yaliyoorodheshwa hapo juu: –
Maonesho ya kazi mbalimbali zinazolenga kuongeza uzalishaji, tija na upatikanaji wa chakula na usindikaji wa mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi;
Kutoa elimu juu ya kuandaa vyakula mbalimbali, lishe bora, uhifadhi na usindikaji wa mazao ya chakula, mifugo na uvuvi katika ngazi ya kaya na jamii.
Kutoa elimu ya matumizi ya mbegu za asili na mchango katika Usalama na Uhakika wa chakula na maendeleo ya Taifa.
Kuhamasisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuwa na ufahamu kuanzisha bustani, ufugaji wa wanyama wadogo wadogo, umuhimu wa lishe bora na ujuzi wa kuandaa mlo kamili.
Kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya vyakula vya asili katika ngazi ya kaya na jamii.
“Ndugu wananchi, kabla ya kuhitimisha taarifa hii ,napenda kutoa shukrani zangu kwa niaba ya Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, kwa wadau wanaoshiriki katika maandalizi ya maadhimisho ya mwaka huu.Wadau hao ni pamoja na Mashirika ya umoja wa mataifa (UN Agencies- FAO,WFP, UNICEF,UNHCR,UNDP), Idara za Serikali na sekta binafsi waliokubali kushiriki kwa kujigharamia na michango mbalimbali ili kufanikisha maadhimisho haya.
“Kwa taarifa hii naomba Viongozi na Wananchi wote kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya ya Siku ya Chakula Duniani mwaka 2021,”amefafanua Waziri Profesa Mkenda.
More Stories
Wahakikishiwa usalama siku ya kupiga kura
CCM inabebwa na kazi nzuri za Rais Dkt. Samia-Makalla
Wananchi Babati wamshukuru Rais Samia kwa kuwafungulia barabara