December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB yatoa mkopo wa mil.436/- ujenzi kiwanda cha kusindika korosho Tanga

Na Mwandishi Wetu, Tanga

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeidhinisha mkopo wa kiasi cha sh. 435,500,000 kwa ajili ya uanzishwaji wa kiwanda kidogo cha kusindika korosho ili kuliongezea thamani zao sambamba na kuongeza pato la taifa pamoja na kuinua pato la mkulima..

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uzinduzi wa mradi wa ubunifu katika mnyororo wa thamani wa zao la Korosho chini ya Taasisi ya Care Tanzania wilayani Mkinga,Jijini Tanga, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa TADB, Jeremiah Mhada alisema benki hiyo imeidhinisha mkopo huo ambapo zitatumika katika ujenzi wa kiwanda na ununuzi wa mashine na vifaa mbalimbali za kuendesha kiwanda hicho.

“Fedha hizo zitatoka kwa awamu ikiwa ni kujenga miundombinu ya kiwanda na awamu ya pili kufadhili wakulima wa korosho pembejeo zitakazowawezesha kuzalisha korosho kwa tija na kupata bei nzuri sokoni,” alisema Mhada

Ameeleza kuwa fedha ziizotolewa zitakwenda kusaidia kutengeneza ajira kupitia kazi ya ujenzi wa majengo ya kiwanda pia kukiwezesha kiwanda Mtaji wa kununua korosho kutoka kwa wakulima wadogo wa Kilimo Viwanda Sigaya Limited.

“TADB imetoa mkopo huu kwa lengo la kuongeza thamani ya zao la korosho hali itakayopelekea kuongezeka kwa mapato ya wakulima wa korosho Wilayani Mkinga,” amesema Mhada na kuongezea kuwa kiwanda hicho kitaongeza thamani ya zao na kuhamasisha wakulima kufanya kilimo cha korosho kutokana na uhakika wa soko.

Mhada amesisitiza kuwa majukumu ya TADB ni kuhakikisha mageuzi yanafanyika katika sekta ya kilimo na kuwabadilisha wakulima kutoka kilimo cha mazoea na kufanya kilimo biashara na kuwafanya waweze kupita hatua kiuchumi kupitia shughuli za kilimo na kuwaunganisha na masoko kupitia chama cha msingi cha ushirika cha DUGA.

“Uchakataji wa korosho hapa nchini utasaidia kuzalisha bidhaa nyingine kama mafuta kwa asilimia 15 ambayo hutumika kama dawa na matumzi ya viwandani jambo litakalopelekea kuongeza thamani ya zao la korosho hapa nchini,” amesema

Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Jeremiah Mhada (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja, huku wakishikilia mfano wa hundi ya mkopo wa shi. milioni 435.5 mkopo ambao benki hiyo imetoa kujenga kiwanda cha kusindika korosho mkoani Tanga. Wengine ni Kanali Maulid Surumbu (Mkuu wa Wilaya Mkinga), Karsten Solaas ( Outgrowers CEO) Projestus Rwehumbiza, Mwagomba ( Mwenyekiti wa Duga AMCOs) Furaha Sichula (Afisa Mwandamizi TADB) Ughumba Kilasa (Mwakilishi wa Bodi ya Korosho mkoani Tanga) Hafla hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki. Na mpiga picha wetu.

Ameeleza kwa sasa mafuta ghafi ya korosho yanauzwa katika soko la Umoja wa Ulaya, Marekani, Japan, Korea ambapo wasambazaji wakuu ni India na Brazil. Hivyo tukiweza kuzalisha wenyewe mafuta haya Tanzania itakuwa miongoni mwa wasambazaji wakuu wa bidhaa hiyo Duniani.

“Kwa mujibu wa ANSAF mwaka 2016/17 Tanzania ni ya tatu kwa uzalishaji wa korosho Duniani, sasa hivi ipo ya nne kwa Afrika ambapo zaidi ya asilimia 90 inasafirishwa kama malighafi,” amesema Mhada

“TADB tutaendelea kuhamasisha kuongeza na kukuza uzalishaji na hii ni muendelezo wa uwekezaji wa zaidi ya bilioni 33 ambazo zimetolewa katika mnyororo wa thamani wa uzalishaji,” amefafanua Mhada

Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha DUGA, Said Tuwano aliishukuru benki ya TADB pamoja na wawekezaji walioamua kuwekeza katika wilaya yao na kusema hii imeonesha dhamira ya dhati ya kusaidia wakulima wadogo nchini.

“Nashukuru zaidi kwa kutupa asilimia 45 ya hisa kwenye kiwanda hivyo zaidi ya wakulima 200 tutakuwa sehemu ya kiwanda na tumejipanga kuhakikisha tunaongeza idadi ya wakulima mpaka kufikia 2,500 katika Wilaya yetu ili tunufaike wote,” amesema Tuwano

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Kanali Maulid Surumbu aliwataka wadau wote kutekeleza majukumu yao kuhakikisha uzalishaji wa zao la korosho unaongezeka pia kuhakikisha kiwanda kinakamilika ili uzalishaji uanze msimu ujao wa mavuno.

“Tunachotaka kutoka kwenu ni uwazi na uwajibikaji, niwahakikishe Serikali ipo pamoja na nyinyi kutoa mchango ili kuhakikisha tija katika uzalishaji inaongezeka na kufanya korosho yetu izidi kukubalika katika soko la ndani na masoko ya kimataifa jambo litakalo ongeza kipato kwa wakulima Wilayani Mkinga,” amesema Kanali Surumbu