Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Dodoma
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeahidi kuendelea kuuunga mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kulifanya Jiji la Dodoma kuwa la kijani ambapo wamewezesha na kufanikisha bonanza la upandaji wa miti 4,000 mwishoni mwa wiki.
Akizungumza katika tamasha la tuzo za Dodoma ya kijani lenye lengo la kutambua mchango wa Taasisi za Serikali, taasisi binafsi, wananchi, shule na vyombo vya ulinzi na usalama vilivyoshiriki katika kuhakikisha Dodoma inakuwa ya kijani kwa kupanda miti, Meneja wa TADB Kanda ya Kati, Yodas Mwanakatwe mbali ya kupongeza mpango huo ambao Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amesema TADB siku zote inajali utunzaji wa mazingira endelevu kama sehemu ya kufanikisha malengo ya kiuchumi.
“Maendeleo ya kilimo na uchumi hayawezi kufikiwa endapo hakutakuwa na utunzaji endelevu wa mazingira, hivyo tunawajibika katika kuchangia kwenye kampuni kama hivi ili nchi yetu iwe na maendeleo sambamba na mazingira salama,” amesema Mwanakatwe.
Amesema katika kufanya shughuli za maendeleo kama kilimo au ujenzi wa viwanda mazingira yanaathirika kwa kiasi kikubwa, hivyo uhamasishaji wa katika mpango wa upandaji wa miti utasaidia katika kutunza na kulinda mazingira yetu.
“Benki ya Kilimo pamoja na kujielekeza kuwezesha maendeleo kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvivu inajihusisha pia katika kuhakikisha mazingira yanalindwa na kutunza ili yaweze kutumika kwa kizazi cha sasa na cha baadae,” amesema Mwanakatwe.
Aidha, ametoa wito kwa wadau wa kilimo,mifugo na uvuvi kuhakikisha wanatunza mazingira yao ikiwa ni pamoja na kupanda miti itakayosaidia kuifanya nchi kuwa ya kijani kadhalika na kusaidia kupunguza hewa ya ukaa duniani.
“Kumekuwa na ongezeko la hewa ya ukaa duniani hii ni kutokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu hivyo katika kukabiliana na hilo ni muhimu kujielekea katika kufanya kampuni kama hivi za kuhamasisha upandaji wa miti,” amesema Mwanakatwe
Ameeleza kuwa TADB itaendelea kutoa mchango wake kwa jamii kuhakikisha mpango wa upandaji miti na kulifanya jiji la Dodoma kuwa ya kijani unatekelezeka kwa vitendo na kusema Dodoma iwe mfano katika kutekeleza upandaji miti mikoa yote nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mpango huo, Waziri mkuu mstaafu Mizengo pinda mbali ya kuipongeza TADB katika kufanikisha kufanyika kwa hafla hiyo ameshauri Serikali kuweka utaratibu maalum kwa kila kaya mkoani Dodoma kuhakikisha inapanda miti mitano ili kukabiliana na hali ya ukame katika jiji hilo.
“Ni muhimu Serikali kuhakikisha inawahamasisha wananchi katika kaya zao kupanda miti angalu mitano na kuitunza ili iwe sehemu ya kuwapatia hewa safi na pia utekelezaji wa mpango wa kuifanya Dodoma kuwa ya kijani,” amesema Pinda
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka amesema upandaji wa miti na uhifadhi wa mazingira ndio kipaumbele cha kwanza katika mkoa huo na kusema amepokea pendekezo la Mwenyekiti wa Kampeni hiyo la kuhakikisha kila kaya inapanda miti mitano kama sehemu ya utekelezaji wa kampeni.
TADB imekuwa miongoni mwa Taasisi za Serikali zilizopatiwa tuzo kutokana na ushiriki wake katika Mpango wa kuifanya Dodoma kuwa ya kijani kwa kuhamasisha upandaji wa miti.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapato