Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online,Shinyanga
WANACHAMA wa Umoja wa Vyama vikuu vya Ushirika vinavyojishughulisha na ununuzi wa zao la pamba nchini (TANCCOP) umeomba kukutana Rais Samia Suluhu Hassan ili wamweleze changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa zao la pamba nchini.
Ombi hilo limetolewa juzi mjini Shinyanga katika uchaguzi mkuu wa kuwachagua viongozi wa kudumu wa umoja huo watakaongoza kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo uliosimamiwa na Kaimu Mrajis vyama vya ushirika mkoani Shinyanga.
Wanachama hao wamesema mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani tayari amekutana na baadhi ya makundi ikiwemo wanawake, wazee, vijana na viongozi wa kidini hivyo kuna umuhimu pia akakutana na wawakilishi wa wakulima nchini vyama vikuu vya ushirika.
Wamesema yapo mambo mengi yanayowakabili wakulima ambayo iwapo watakuna na Rais Samia watamweleza na kutokana na nafasi yake ataweza kuyatolea ufafanuzi na hata kuagiza ili yarekebishwe hivyo kuondoa changamoto kadhaa zinazowakabili wakulima hasa wa zao la pamba.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Singida (SIFACU), na ambaye ni mjumbe wa Bodi ya TANCCOP, Yahaya Khamis amesema wakulima wa mazao makuu ya kibiashara bado wana changamoto nyingi katika kilimo cha mazao yao hasa upande wa bei kwenye masoko.
Khamis amesema upande wa wakulima wa zao la pamba wanakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakati na hata pale zinapopatikana bei zake huwa siyo rafiki kwa mkulima vivyo hivyo upande wa bei pale wanapouza pamba yao.
“Sasa iwapo tutakutana na Rais wetu, tutaweza kumweleza changamoto hizi na kushauriana naye jinsi gani ataweza kuzipatia utatuzi ili mkulima wa zao la pamba ama wale wa kahawa na korosho watakavyowezeshwa kupata pembejeo za kilimo kwa wakati na kwa bei rafiki,” ameeleza Khamis.
Kuhusu mfumo wa uuzaji mazao ya biashara kwa utaratibu wa Stakabadhi za ghala alisema mfumo huo ni mzuri na una faida kubwa kwa wakulima iwapo utasimamiwa kikamilifu na kutekelezwa kama inavyotakiwa japokuwa mpaka sasa wapo baadhi ya watu wanaoupinga kwa maslahi yao binafsi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Kahama (KACU) Geoffrey Mbuto amesema mara baada ya kupatikana kwa uongozi wa kudumu wa TANCCOP kuna umuhimu wa kumuomba Rais Samia aweze kukutana nao.
“Tunaomba ikiwezekena TANCCOP tupate fursa ya kukutana na Rais wetu, ili tuweze kumfikishia kilio cha muda mrefu cha mkulima wa zao la pamba hapa nchini kuna changamoto zilizopo zinazokwamisha ufanisi katika suala zima la kilimo chao pamoja na kusuasua kwa bei ya zao hilo kila mwaka,” ameeleza Mbuto.
Mbuto ameshauri iwapo itawezekana, TANCCOP iruhusiwe kushughulikia usambazaji wa viuatilifu na pembejeo za kilimo kwa wakulima wa zao la pamba na pawekwe utaratibu utakaowawezesha kupatiwa mikopo kutoka katika mabenki hapa nchini.
Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoani Shinyanga, Hilda Boniface aliyekuwa msimmazi katika uchaguzi huo amewataka viongozi waliochaguliwa kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa kuzingatia kanuni zilizomo ndani ya masharti yao Umoja wao.
“Mbali ya kukupongezeni viongozi wapya mliochaguliwa, lakini niwaombe anzeni kazi zenu kwa kupitia madhumuni yote ya uanzishwaji wa TANCCOP, ambamo mna kila kitu, dira na mambo yote yamo, kumbukeni ushirika unaongozwa na kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu pamoja na sheria ndogo ndogo mlizojitungia,” ameeleza Hilda.
Katika uchaguzi huo,Zainab Mahenge kutoka Geita Cooperative Union amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa TANCCOP, Deogratias Didi kutoka Chato, alichaguliwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa umoja huo.
Wajumbe watatu waliochaguliwa ni pamoja na Godffrey Mbuto kutoka Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Kahama, KACU, Ramadhani Yahya kutoka SIFACU Singida na Makutano Mboje kutoka SIMCU Simiyu na Kaimu Katibu Mkuu ni Ramadhani Katto.
“Matarajio ya kuanzishwa wa umoja huu ni kuwezesha kutetea maslahi ya wakulima wa zao la pamba nchini ikiwemo suala la bei, sasa hivi tuna mwaka mmoja na nusu tangu umoja huu ulipoasisiwa, lakini tayari tumewezesha kupatikana kwa bei nzuri ya pamba katika msimu wa mwaka huu,” ameeleza Katto.
Umoja huo unaundwa na vyama 12 vya ushirika kutoka mikoa ya Shinyanga (SHIRECU na KACU), Geita (GCU), (CCU – Chato) na MBCU), Mwanza (NCU), Simiyu (SIMCU), Tabora (Igembensabo), Singida (SIFACU na SIAMCU Manyoni), Katavi (LATCO Ltd) na Mara (WAMACU).
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea