November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampuni yazindua kinywaji cha Kiwingu

Na Bakari Lulela

KAMPUNI ya Kilimanjaro Biochem Limited, imezindua rasmi kinywaji kipya aina ya Kiwingu ambacho huzalishwa nchini na kusambazwa Mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.

Akizungumza katika uzinduzi huo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exand Kigahe ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema serikali itaendelea kuunga mkono wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, ili kufanikisha mikakati ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

“Nawapongeza Kilimanjaro Biochem Limited kwa kuzindua kinywaji kiitwacho Kiwingu kuingia sokoni sambmba na mikakati yao ya kuyateka masoko zaidi, tumejumuika pamoja na wafanyabiashara katika tukio hili,” amesema.

Naibu Waziri huyo, amesema uwepo wa malighafi nyingi katika sekta ya kilimo yameleta mabadiliko na manufaa makubwa kwa Watanzania na kwa wawekezaji kutambua fursa zilizopo nchini zitokanazo na bidhaa ya kinywaji hicho.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kilimanjaro Biochem, Mehul Patel amesema soko la vinywaji nchini lina ushindani mkubwa, ambapo wao wazalishaji wanajali ubora na kuhakikisha kunakuwa na viwango vya hali ya juu, ambavyo hutengenezwa kwa kutumia ethanol.

Patel amesema kampuni hiyo, imewekeza kwa takribani sh. bilioni 11.5 kwa ajili ya uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa hiyo mpya itakayosaidia uchumi kwa kutoa ajira kwa Watanzania, ambapo 200 katika ajira rasmi na zaidi ya 50 kwenye ajira zisizo rasmi.

Kampuni ya Kilimanjaro Biochem, inashirikiana na jamii kupitia programu ya uwajibikaji wa huduma za kijamii (CSR) kwa kutoa kiasi cha sh. milioni 24 kila mwaka na kuziweka kwenye sekta ya elimu, afya na maji.