Na Lulu Mussa, TimesMajira Online,Ruvuma
NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Hamad Chande amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Bi. Tina Sekambo kuhahikisha anafanya ukarabati haraka wa mfumo wa maji taka katika machinjio ya Manispaa ya Songea ili kulinda mazingira.
Chande ameyasema hayo jana mara baada ya kufanya ziara ya kikazi kukagua uzingatia na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 katika Mkoa wa Ruvuma.
Akiwa katika machinjio hayo Naibu Waziri Chande amesikitishwa na namna machinjio hiyo inavyoendeshwa kwa kushuhudia usafi wa mazingira usioridhisha ikiwa ni pamoja na utiritishaji wa maji taka katika mtaro usio rasmi, kutapakaa kwa damu katika sakafu na kushuhudia watumishi wakifanya kazi bila vifaa vya usalama mahali pakazi.
Chande ametoa muda wa siku saba kwa uongozi wa Machinjio hiyo kurekebisha dosari zilizojitokeza na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Songea Bw. Pololet Mgema kufuatilia utekelezaji wa maelekezo hayo na kutoa mrejesho mapema.
Awali, Naibu Waziri Chande pia ametembelea Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Songea na kutoa rai kwa Uongozi wa Wilaya kusikiliza na kupatia ufumbuzi changamoto za wakazi wanaozunguka maeneo hayo ili wawe walinzi wa mazingira na miundombinu inayozunguka vyanzo hivyo.
“Ndugu zangu, maji ni uhai natoa rai kwenu kulinda vyanzo vya maji katika milima hii ya Matogoro kwa kudhibiti shughuli za kibinadamu zisizoendelevu” Chande alisisitiza.
Akitoa taarifa ya hali ya Mazingira katika Mkoa wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Willbert Ibuge amesema Mkoa unakabiliwa changamoto za Kilimo cha kuhamahama, uchomaji holela wa mkaa, uvamizi na uchomaji wa misitu.
Amesema jitihada zimefanyika kwa kushirikiana na wadau wa Mazingira ili kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wavamizi wote waliopo kwenye hifadhi za misitu zikiwemo za Bonde la Rufiji.
Naibu Waziri Hamad Chande yuko Mkoani Ruvuma katika ziara ya Kikazi ya kukagua Utekelezaji na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004. Katika siku ya kwanza ya ziara yake amefanya ukaguzi katika Manispaa ya Songea na siku ya kesho atakuwa Wilayani Mbinga.
More Stories
Mwalimu adaiwa kumfanyia ukatili mwanafunziÂ
NAOT watakiwa kuendana na viwango vya ukaguzi
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu