November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yaja na utaratibu mpya wa kuweka akiba

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Dar

BENKI ya NMB imekuwa ya kwanza nchini kumuwezesha mteja kuweka akiba kila anapofanya miamala kwa kuzindua huduma maalumu kwa ajili hiyo inayojulikana kama “Spend to Save – Miamala Yako ni Akiba Yako” kupitia waleti maalumu.

Huduma hiyo mpya na ya kipekee iliyozinduliwa rasmi Ijumaa iliyopita kwenye makao makuu ya benki hiyo ni kwa ajili ya akaunti binafsi, akaunti za chap chap na akaunti za mwanachuo.

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Bw. Filbert Mponzi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye hafla ya uzinduzi wa bidhaa mpya ya Benki ya NMB ‘SPEND 2 SAVE’ leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa, Aloyce Maro pamoja na Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya NMB, Ally Ngingite wakishuhudia tukio hilo. Katika huduma hiyo mteja aliyejiunga atanufaika na faida kadri anavyofanya matumizi yake.

Wakizungumza wakati wa uzinduzi wake, maofisa waandamizi wa NMB walisema kuanzishwa kwa huduma hiyo ni mapinduzi makubwa ya jinsi ya kuweka akiba na kuwahamasisha Watanzania kutunza fedha kwa ajili ya matumizi ya baadae na kufanya uwekezaji.

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Bw Filbert Mponzi, amesema “Spend to Save” pia inadhihirisha ubunifu wa hali ya juu wa NMB na uongozi wake wa kuanzisha suluhishi wezeshi za kibenki.

Pia ni udhibitisho tosha wa kuwa kinara wa kuwahudumia Watanzania na kuwa mtari wa mbele kuwahamasisha kujenga utamaduni wa kuweka akiba, aliongeza.

Naye Mkuu wa Idara ya Bidhaa, Aloyse Maro, amesema huduma hiyo mpya pia inaongeza namna bora ya kuwahudumia wateja.

“Hili ni jambo kubwa kipindi hiki tunapowakumbusha Watanzania na wateja wa NMB kujitunzia akiba kwa maisha ya baadae,” Bw Mponzi amesema.

“Huduma hii ni ya kwanza na ya aina yake kuwahi kutokea nchini Tanzania ambapo mteja anajitunzia fedha zake kupitia miamala yake anayoifanya iwe kununua kitu, kutoa fedha kutoka kwenye akaunti yake au hata kutuma fedha,” alifafanua.

Huduma ya “Spend and Save” inapatikana kwa mteja kujisajili kupitia zaidi ya ATM 8,000 za NMB zilizotapakaa nchi nzima na kuweka malengo kwa asilimia ya kila muamala anaoufanya.

Mponzi amesema kiasi kitakachokatwa kwa ajili ya akiba ni kati ya asilimia mbili hadi kumi ya kila muamala utakaofanyika na miamala itakayohusika ni ile inayofanywa kupitia ATM, POS, NMB Direct au NMB Mkononi.

“Tunapanua wigo wa akaunti zetu binafsi ili kuwawezesha wateja wetu kuwa na maaumuzi zaidi katika kusimamia fedha zao kwani huduma hii ina faida nyingi sana ambazo zitamsaidia mteja kuwa na tabia ya kujiwekea akiba na kufanya matumizi yenye malengo,” alifafanua.

Mponzi amesema Benki ya NMB imeanzisha utaratibu huu baada ya kugundua kuwa wateja wake wengi hawana tabia ya kuweka akiba na hivyo kuona umuhimu wa kuwaletea huduma ambayo itawasaidia kuweka akiba mara kwa mara na kwa malengo.

Aidha, uzuri wa huduma hii ni pia mteja kuweza kutoa fedha zake kutoka kwenye waleti na kuzirudisha kwenye akaunti muda wowote na atakapofanya hivyo ataruhusiwa kutoa mpaka asilimia 50 ya fedha iliyohifadhiwa. Pia mteja anaweza kujitoa kwenye wallet na fedha zilizohifadhiwa zitarudishwa kwenye akaunti mama.

“Huu ni muendelezo wa huduma ambazo NMB tumekuwa tukianzisha ili kusaidia wateja wetu kwa kutoa suluhisho za huduma za kibenki zenye tija hapa nchini na kutufanya kinara wa kufanya hivyo,” Bw Mponzi aliwaambia waandishi wa habari kwenye uzinduzi wa “Spend and Save”.