Grace Gurisha, TimesMajira Online
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kufadhili vifaa vya kufundishia kozi ya uhandisi wa matengenezo ya ndege kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambacho vinathamani ya Sh. milioni 245.4.
Vifaa hivyo vinagharimu fedha nyingi za walipa kodi, hivyo Chuo kinatakiwa kuvitunza ili viwenze kuwasaidia wanafunzi katika kutimiza malengo yao.
akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo katika Chuo hicho, Profesa Ndalichako amesema hiyo ni moja ya jitiada za Serikali kuhakikisha vyuo vikuu vya mikakati vinatoa mafunzo kwa weledi.
“Vifaa hivi ni vya kisasa na vyenye ubora wa hali juu, naamini vitakidhi mahitaji ya taaluma hapa chuoni na pia tunategemea vifaa hivi vitaongeza Chuo kutoa mafunzo kwa vitendo kwa weledi,” amesema Profesa Ndalichako.
Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Geuzye amesema, makabidhiano hayo ya vifaa hivyo ni vya mafunzo kwa ajili ya Shule Kuu ya Anga katika kuboresha mafunzo ya utengenezaji wa ndege hapa nchini.
Amesema, ununuzi wa vifaa hivyo unefanikiwa kupitia ruzuku ya Sh. 245,466,729.45 iliyotolewa na Wizara hiyo kupitia Mfuko wa Elimu Taifa baada ya NIT kuwasilisha maombi ya ruzuku kwa ajili ya vifaa hivyo.
“Ruzuku iliyotolewa kwa NIT ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la msingi la mfuko huu unaosimamiwa na mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA),” amesema
Geuzye amesema, lengo ni kuongeza jitiada za Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wa mafunzo kwa vitendo.
Kupitia ufadhili huo, mkurugenzi huyo amesema ni wazi kuwa vijana wengi wa kitanzania wenye ndoto za kuwa wataalamu katika sekta ya usafiri wa anga watafikia ndoto kwa kupata mafunzo yao hapa nchini kwa gharama nafuu.
“Sote tunafahamu kuwa ili nchi kupiga hatua zaidi za kiuchumi ni lazima iwe na mfumo mzuri wa usafirishaji ikiwa pamoja na usafiri wa anga”, amesema Geuzye.
Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Zacharia Mganilwa amesema kuwa, vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi katika mafunzo ya wahandisi wa ndege ambapo vinakwenda sambamba na ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga.
Pia, Profesa ameiomba serikali kuwapunguzia ruzuku kwa asilimia 50 kwa 50 ili kuwepo na unafuu wa uendeshaji wa mafunzo katika chuo hicho.
Amesema, wanafunzi hao wanalipa Sh. milioni sita kwa mwaka, ambapo wangeenda kusoma nje wangelipa Sh milioni 200 hadi 300 kwa hiyo wameokoa fedha nyingi kwa sababu mafunzo mengi wanayapata hapa nchini.
Aidha, Mkuu huyo ameiomba Serikali kuwafanyia mchakato wanafunzi wanaosoma diploma na wao waweze kupata ufadhili kwa sababu wao hawana kabisa na ada yao ni Sh milioni tano.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia