Na Esther Macha,TimesMajira Online ,Mbeya
KATIKA kuhakikisha kundi la watu wenye ulemavu wa kusikia (Viziwi)wanajikinga na virusi vya corona hospitali ya Rufaa ya kanda imeanza kutoa elimu kwa kundi hilo ili waweze kujikinga na ugonjwa huo hatari .
Akizungumza na majira juzi ofisini kwake Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ,Dkt .Godlove Mbwanji amesema kuwa mbali ya kutoa elimu kundi hilo pia wameweza kutoa kutoa elimu kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo.
“Kulingana na ulemavu wa kusikia walionao kundi hili (Viziwi) hospitali imeona kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa kundi hili ili wajue namna mbalimbali za kujikinga,hata wataalam wetu hapa ambao wanahudumia kundi hili tumeona kuna umuhimu wa kutoa elimu kwao”amesema mkurugenzi huyo.
Dkt. Mbwanji amesema kwamba wameona ni muhimu kutoa elimu kwa kundi hilo kutokana na hali halisi ya mazingira ya watu wenye ulemavu wa kusikia ilivyo.
“Ni muda mwafaka kusaidia kundi hili ili lisiweze kuangamia na gonjwa hili hatari ,tumejitahidi kuwakusanya kwa pamoja na kuwapa elimu hii muhimu kwao ili waweze kujikinga”amesema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa kusikia Mkoa wa Mbeya (Viziwi)Tusa Mwalwega amesema kuwa wanashukuru hospitali hiyo kujali kundi hilo na kuona kuwa lina umuhimu katika jamii.
“Tunashukuru Sana mkurugenzi wa hospitali kwa kutujali maana wengi wetu tulikuwa tupo tupo hivyo ingeweza kuwa hatari katika kipindi hichi ambacho ugonjwa huu umepamba moto,maana tumemsikia hata mh Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan akisema hali ni mbaya akitutaka watanzania kuendelea kufuata maelekezo ya wataalam pamoja na kujikinga kwa kutumia barakoa na kuepuka misongamano”amesema Mwalwega.
Akizungumza na gazeti hili ,Mkalimani wa lugha za alama Mkoa wa Mbeya ,Faraja Mbwilo amesema kuwa hospitali ya Kanda ya rufaa imekuwa msaada mkubwa katika kuwasaidia viziwi ,lakini changamoto bado ipo kwa maeneo ya vijijini ambako nako kuna kundi hilo kubwa la watu wenye ulemavu wa kusikia.
Hata hivyo amesema ombi kwa taasisi zingine zisizokuwa za kiserikali nazo zione umuhimu wa kusaidia kundi hilo katika mapambano dhidi ya corona ,kuna viziwi wapo vijijini wanahitaji msaada mkubwa katika Vita ya kupambana na gonjwa hatari law Corona.
Aidha Dkt.Mbwanji amesema kuwa mbali na kutoa mafunzo hayo hospitali imechukua tahadhari nyingine ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano wodini kwa kuruhusu watu wachache kuingia wodini kuona wagonjwa.
Amesema kuwa kwa kuanzia walianza kutoa elimu kwa ndugu wa wagonjwa katika kupunguza idadi ya ndugu ambao wanakuja kuona wagonjwa ambao wataingia ndugu wawili kila wakati kwa kupeana nafasi ya kuingia kwa kadi maalum pamoja na kunawia dawa ya vitakasa mikono.
Hata hivyo Dkt. Mbwanji amesema hivi sasa kila mmoja amechukua tahadhari ya kupambana na ugonjwa huu kwa kunawa mikono pia kuweka vitakasa mikono maeneo ya ofisi na biashara yakiwemo masoko.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia