Na Munir Shemweta, WANMM
NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula amewataka wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani waliorasimishiwa makazi yao kutumia fursa ya Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa kujipatia hatimiliki za ardhi zinazopatikana ndani ya siku moja katika maonesho hayo.
Akizungumza wakati wa kutembelea Banda la Wizara ya Ardhi katika maonesho hayo katika viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa Dar es Salaam, Dkt. Mabula amesema, maonesho ya Sabasaba ni fursa nzuri kwa wananchi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani kujipatia hatimiliki za ardhi pamoja na huduma nyingine za sekta hiyo kwa uharaka zaidi.
Katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya mwaka huu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inatoa hatimiliki za ardhi kwa wale wananchi waliorasimishiwa makazi yao na kuwa na nyaraka muhimu kupata hati ndani ya siku moja.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mabula, kasi ya serikali ya awamu ya sita ni kubwa na sasa hatimiliki ya ardhi inapatikana kwa siku moja tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo pamoja na mmiliki kuwa nyaraka zote lakini kupata hati ilikuwa vigumu.
“Kasi ya serikali ya awamu ya sita ni kubwa sana katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inapatiwa ufumbuzi na kwa kuwa hivi sasa tuko katika mfumo wa kidigitali hatimiliki ya ardhi unaweza kuipata ndani ya muda mfupi kwenye banda la wizara hapa sabasaba tofauti kabisa na miaka ya nyuma,”amesema Dkt Mabula.
Naibu Waziri Dkt Mabula ambaye alikabidhi hati za ardhi kwa baadhi ya wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Ardhi katika maonesho hayo ya 45 ya Biashara ya Kimataifa alisema, hata wale wananchi wenye migogoro ya ardhi wanaweza kupata ufumbuzi wa migogoro papo hapo kupitia wataalamu wa sekta ya ardhi waliopo kwenye maonesho.
Akielezea zaidi utendaji wa Wizara yake, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema kuwa, Wizara ya Ardhi imejipanga vizuri kuhudumia wananchi kutokana na huduma za sekta hiyo kupatikana kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
‘’ Yeyote mwenye changamoto ya ardhi kwa sababu huduma zinafanyiika hapa kwa karibu afike katika maonesho ya SABASABA atapata ufumbuzi wa suala lake maana watumishi wapo kwa ajili ya kufanya kazi na hata waliopo mikoani huduma inatolewa huko ambako ni sawa na Wizara ya ardhi,’’alisema Dkt. Angeline Mabula.
Baadhi ya wananchi waliopata hatimiliki za ardhi zilizotokana na zoezi la urasimishaji katika maonesho hayo walipongeza Wizara ya Ardhi kwa kufanikisha kutoa hati ndani ya muda mfupi katika maonesho ya Sabasaba na kutaka kazi hiyo iendelee na kwenye mikoa mingine hata baada ya maonesho hayo.
‘’Hatua hii ya kutoa hati ndani ya muda mfupi ni nzuri sana na inatakiwa iwe endelevi isiwe katika maonesho pekee na ifanyike pia katika mikoa mingine ili kuwaondolea usumbufu wanannchi wanaotaka kupata hati,’’ amesema Ally Ismail mkazi wa Gongolamboto.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria