Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
HATMA ya uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka hapa nchini (TFF) uliopangwa kufanyika Agosti 8, jijini Tanga itajulikana kesho baada ya leo Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kupokea kesi ya kupinga uchaguzi huo.
Kesi hiyo imefunguliwa na aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Urais, Ally Saleh ambaye amelalamikia mchakato wa uchaguzi huo pamoja na muundo wa shirikisho hilo katika uchaguzi huo.
Kabla hata ya kuenguliwa katika mchujo wa awali kwa kukosa sifa ikiwemo ya kutokidhi takwa la kikanuni la kutakiwa kuwa na wadhamini angalau watano, Saleh alikuwa tayari ameshaandika barua kwenda kwenye Kamati ya uchaguzi ili kuomba mambo kadhaa yafanyiwe marekebisho ikiwemo siku za kusaka wadhamini.
Pia Salehe alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya Habari akiwa kwenye mkutano akidai kama Zanzibar ni sehemu kamili ya Jamhuri ya Muungano basi inapaswa kushirikishwa katika uchaguzi huo la sivyo katiba yao isitishwe ili warudi kwenye meza ya majadilizno kuangalia ni kwa nanna gani wanaweza kushirikishwa kwenye shughuli za TFF.
Kwa mujibu wa Mwanasheria, Frank Chacha anayemtetea, Salehe amesema, kesi hiyo namba 98 itaanza kusikilizwa leo na kikubwa ambacho mteja wake amekilalamikia ni kanuni za uchaguzi na muundo wa TFF kutoitambua Zanzibar katika mchakato wa uchaguzi.
Wakili huyo ameweka wazi kuwa, tayari wahusika wote wanaolalamikiwa kwenye shauri hilo wameshapelekewa wito wa Mahakama Kuu wakitakiwa kufika leo saa 3 asubuhi.
Haya yanatokea ikiwa tayari Kamati ya Uchaguzi imeshamtangaza Wallace Karia kuwa mgombea pekee katika nafasi ya rais baada ya wapinzani wake kukosa vigezo hivyo sasa ni kipindi cha Sekretarieti kuwasilisha masuala ya kimaadili kwenye kamati ya maadili huku Julai 3 hadi 7 kitakuwa ni kipindi cha kupokea, kusikiliza na kutolea uamuzi masuala ya maadili.
Pia Kamati ya maadili ya TFF itatangaza matokeo ya uamuzi Julai 10 na Julai 11 hadi 13 kitakuwa ni kipindi cha kukata rufaa kw uamuzi wa masuala ya kimaadili kwenye kamati ya Rufani ya TFF, Julai 14 hadi 18 kitakuwa ni kipindi cha kusikiliza rufani ambapo kipindi cha kukata rufani dhidi ya kamati ya uchaguzi kitaanza Julai 22 hadi 24 na zitasikilizwa kati ya julai 24 na 28.
Wagombea na Kamati ya uchaguzi watajulishwa uamuzi wa Kamati Julai 29 na 30 orodha ya mwisho ya wagombea itatolewa na kisha kampeni zitafunguliwa Agosti Mosi hadi 6 na uchaguzi rasmi utafanyika Agosti 7.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship