November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ufanisi TPA warejesha matumaini sekta Binafsi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dar

TAKRIBANI miezi mitatu tangu Rais Samia Suluhu Hassan afanye mabadiliko ya uongozi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Tangu kufanyika mabadiliko hayo ufanisi umeshaonekana, kwani huduma zimeboreshwa na kufanya sekta bianfsi kuridhishwa na utendaji kazi wa bandari ambayo ndiyo lango kuu la biashara.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta bianfsi Nchini (TPSF), Angelina Ngalula amepongeza utendaji kazi wa Mamlaka ya Bandari na kusema kuwa matarajio ya wadau na watumiaji wa bandari ni kuona huduma Bora na ufanusi.

“Tunapongeza hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na TPA kuhakikisha mizigo bandarini inaondolewa kwa wakati bila ya ucheleweshaji wowote,” amesema Ngalula

Amesema matokeo chanya ya muda mfupi yametokana pia na kamati iliyoundwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwa kushirikisha wadau na mamlaka kuweza kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinakwamisha ufanisi bandarini.

“Changamoto kubwa ilikuwa ni uratibu hivyo kuundwa kwa Kamati ya uboreshaji wa bandari(PIC) ambayo inaongozwa na Katibu Kuu Wizara ya uchukuzi imeleta mafanikio makubwa kwa muda mfupi, “ amesema Ngalula

Ameeleza kuwa kupitia PIC kumekuwa na ushirikiano mkubwa kati ya taasisi zote za umma na bianafsi zinazotoa huduma bandarini na kupelekea bandari kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa hali inayopelekea biashara ya usafirishaji kuongezeka katika bandari yetu.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta bianfsi Nchini (TPSF), Angelina Ngalula

“Serikali imefanya kazi kubwa katika kupunguza kodi mbalimbali ambazo zilikuwa kikwazo katika kuifanya bandari kufanya kazi kwa ufanisi,” alisema Ngalula na kuongezea kuwa ufanisi uliopo utaendelea kuifanya Bandari kuchangia pakubwa katika pato la Taifa na kuifanya nchi kupiga hatua kiuchumi.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR utapelekea ufanisi wa badari yetu kuongezeka zaidi kwani reli hii itasaidia kuondosha mizigo bandari kwa kiwango kikubwa na kupelekea msongamano wa mizigo bandarini kupungua kabisa.

Katika Hatua nyingine, Ngalula amemuomba Rais Samia kutazama upya mradi wa Bandari ya Bagamoyo kutokana na nafasi ndogo iliyopo katika Bandari ya Dar es Salaam haiwezi kupokei meli kubwa zinazoundwa kwa kizazi cha sasa, hivyo kuna umuhimu kubwa wa kuangalia upya mradi huu.

“Kuna kila sababu ya kutazama upya mradi huu kwani meli za kizazi cha nne ni kubwa kulinganisha na meli za zamani, hivyo bandari hii itaweza kutuweka katika ushindani na nchi nyingine katika kupokea meli kubwa za mizigo, “amesema Ngalula

Bandari ya Dar es Salaam

Akijibu hoja za Mwenyekiti za TPSF katika mkutano wa 12 wa Baraza la Taifa la Biashara(TNBC), Mwenyekiti wa Mkutano huo, Rais Samia Suluhu Hassan alisema mchakato wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo unaendelea, Serikali inafanya mazungumza na mwekezaji na pia kupitia upya masharti yaliyopo katika mkataba huo.

“Lengo letu ni kuboresha mazingira ya uwekezaji ili mradi huu uweze kunufaisha pande zote mbili ikiwa ni pamoja na kutengeneza ajira kwa vijana na kupelekea uchumi kukua,” amesema Rais Samia