November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 3.4 kusambaza maji ya bomba Mara

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online, Mara

JUMLA ya shilingi bilioni 3.4, zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya miradi ya usambazaji wa maji ya bomba kutoka ziwa Victoria kwenda vijiji mbalimbali vya wilaya ya Musoma mkoani Mara.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA wa wilaya hiyo, Mhandisi Edward Silonga na kufafanua kuwa Sh bilioni 1.3 ni fedha zinazotokana na bajeti ya mwaka 2020/2021.

Meneja huyo amesema jana kuwa Sh. bilioni 2.1 ni za bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 ambazo zitatumika kuendeleza kazi ya kuboresha miundombinu ya maji katika wilaya hiyo.

“Katika bajeti mbili, serikali ilitutengea Sh. bilioni 3.4 kusambaza maji ya bomba kutoka ziwa Victoria kwa ajili vijiji vyote 68 vya wilaya ya Musoma ili kuhakikisha kila kijiji kinapata maji safi na salama,” amesema Silonga.

Amefafanua kuwa, baadhi ya miradi ya maji ukiwamo wa Kijiji cha Bukima umekamilika kwa fedha za bajeti ya mwaka 2020/2021, huku mingine ikiwa katika hatua ya mwisho na baadhi ikiwa ikiendelea kufanyiwa kazi.

Meneja huyo aliutaja mradi wa maji wa vijiji vya Makojo na Chitare kuwa umeshatekelezwa kwa asilimia 90, na kwamba kufikia Juni 30 mwaka huu, utakuwa umekamilika.

“Kazi zilizokamilika katika mradi huu ni ujenzi wa mtambo wa kusukuma maji kutoka kwenye chanzo na kuweka mtandao na kuweka mabomba yenye urefu wa kilomita 18 na ufungaji wa mfumo wa umeme,” amesema.

Ameongeza kuwa kuna ufungaji wa vitekea maji 18, ujenzi wa vioski vinne, ujenzi wa matangi matatu likiwamo lenye uwezo wa kuchukua lita 100,000 za Kwikonero, Rwanga na Kasoma wenye thamani ya Sh. milioni 80.

“Lakini pia ya kuna mradi wa maji wa vijiji vya Butata na Kastamu ambao gharama yake ni Sh. milioni 286.1, jumla ya gharama za miradi hiyo yote ni Sh. milioni 450.1, zinazotokana na bejeti ya mwaka 2020/2021,” amesema.

Mhandisi huyo amefafanua RUWASA inaendelea kutandaza miundombinu ikiwamo ya pampu za kusukuma maji kwenda vituo mbalimbali vya vijiji ambavyo viko mbali na ziwa Victoria ili viweze kupata huduma hiyo.