Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online,Lindi
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza korosho zote zinazozalishwa katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi zisafirishwe kupitia badari ya Mtwara kwani serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika bandari hiyo kwa kuikarabati na kuipanua.
Amesema hayo jana wakati wa kikao na wadau wa zao la korosho kilichofanyika mjini Lindi.
Amesema kuwa Rais Samia amewaagiza viongozi wa bandari wapitie tozo zote zinazowakwaza wasafirishaji ili kuwavutia kuitumia bandari hiyo “tunataka wasafirishaji watumie bandari hii kusafirisha korosho kuanzia na msimu huu”.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa wakulima wakubali kupokea pembejeo kulingana na mahitaji yao na watalipia kulingana na idadi ya mifuko waliyochukua na sio shilingi 110 kwa kila kilo kama inavyelezwa “kila kilo ni gharama mno, lengo letu ni kuendelea kumpungumzia mzigo mkulima, msiogope kuchukua pembejeo”
Waziri Mkuu ametoa wito kwa wakulima wa zao la Korosho kuwa na utaratibu wa kubangua korosho ili kupata faida zaidi badala kuziuza bila kuzibangua “tungebangua wenyewe tungepata faida kubwa sana, wenye viwanda panueni viwanda vyenu na kukuza mitaji na wakulima wadogo endeleeni kubangua ili kuongeza thamani ya korosho zetu.”
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono wadau wote wa korosho nchini katika kufanikisha mkakati huo ikiwemo kutengeneza mashine za ubanguaji kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) “ni vyema tujikite kwenye ubanguaji kuliko kuisafirisha nje ya nchi ikiwa ghafi, tumeandaa mfumo mzuri na Rais wetu ameendelea kusisitiza katika ujenzi wa viwanda”.
Akiongelea tozo ya unyaufu, Waziri Mkuu amesema kuwa tozo hiyo haikubaliki kwa kuwa haina uhalisia kwani hata sheria na kanuni kwenye Wizara ya kilimo haitambui unyaufu. “tusisikie makato ya unyaufu kwasababu yanawafanya wanunuzi wahisikuwa wanaonewa, viongozi wa Serikali tusimamie hilo, hatutaki kusikia kuhusu tozo ya unyaufu”
Vilevile Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inaweka mpango wa kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na Afisa Ugani mmoja atakayesaidia kutoa elimu kwa wakulima juu ya namna bora ya kusimamia mazao yao ili kuongeza tija.
“wakulima wanakosa elimu ya namna ya kuliendesha zao hili, maafisa kilimo mlioko maofisini tokeni muende vijijini kuwaelimisha wakulima namna bora ya kulima mazao, wakati wote mnatakiwa kuwa shambani kuhakikisha wakulima wanalima kwa kuzingatia miongozo ya kilimo bora”.
Naye Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Wizara hiyo itaendelea kubuni na kusimamia mikakati itakayoongeza tija katika zao la korosho kwa kutoa pembejeo sahihi na kwa wakati lengo likiwa ni kukidhi mahitaji ya masoko duniani .
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Taleck amesema kuwa atashirikiana na viongozi wa mikoa ya Ruvuma na Mtwarakuhakikisha kwamba minada yote ya korosho inafanyika kwa uaminifu na uadilifu mkubwa ili kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Mbunge wa Jimbo la Tandahimba Katani Ahmad Katani amesema kuwa amefarijika na kauli ya Serikali kuhusu korosho zote kusafirishwa kupitia bandari ya Mtwara kwani itasaidia kuongeza fursa za maendeleo katika mikoa ya kusini.
Akichangia katika mjadala huo, Mkulima wa Korosho kutoka Tunduru Shaibu Hassan amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuondoa tozo ya shilingi 110 kwa kila kilo moja ya korosho ghafi inayouzwa kwa ajili ya pembejeo, “kero yetu kubwa ilikuwa ni kilo moja ya pembejeo uchukue salfa au usichukue, huu ndio ujumbe mzito ambao Mama Samia ametupatia sisi wakulima wa korosho”.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa