November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia afanya ziara ya kushtukiza

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Juni 1, 2021 amefanya ziara ya kushtukiza kwa kutembelea masoko ya Kariakoo na Kisutu, mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya pili na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala Mkoani Dar es Salaam.

Katika Soko la Kariakoo, Mhe. Rais Samia amewatembelea wafanyabiashara wanaouza bidhaa zao hasa vyakula ndani ya soko kuu na kujionea msongamano mkubwa wa bidhaa, wafanyabiashara na wananchi wanaokwenda kununua bidhaa.

Wafanyabiashara hao wamelalamikia tatizo la ugumu wa uingizaji wa bidhaa kutokana na njia za kuingia sokoni kufungwa na wafanyabiashara wengine ambao wamepanga bidhaa zao njiani, tozo kubwa za vizimba,  ushuru wa bidhaa zinazoingia sokoni na gharama za usafishaji wa bidhaa kutoka masoko mengine.

Baada ya kujionea hali halisi, Mhe. Rais Samia ameelezea kusikitishwa kwake na hali hiyo na amesema Serikali itafanya tathmini ya uendeshaji wa soko hilo ili kurekebisha dosari zilizopo ikiwemo kuratibu uingizaji wa mizigo, mpangilio wa bidhaa sokoni na kuboresha usafi.

Ameagiza kusimamishwa mara moja kwa uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo ili kupisha uchunguzi kufuatia malalamiko mbalimbali yaliyotolewa na wafanyabiashara dhidi ya viongozi hao, lakini wakati hatua hizo zinachukuliwa amewataka wafanyabiashara kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu na sheria.

Katika soko la Kisutu, Mhe. Rais Samia amejionea kazi za ukamilishaji wa soko hilo ambalo linatarajiwa kukamilika wiki ijayo na kuwarejesha wafanyabiashara waliokuwa wameondolewa kupisha ujenzi wake.

Mhe. Rais Samia amekagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya pili kwa kutembelea maeneo ya Mbagala Rangi Tatu na Mbagala Zakhem ambapo kazi za ujenzi zimefikia asilimia 16 badala ya asilimia 60 iliyotarajiwa.

Akiwasalimu wananchi wa Mbagala, Mhe. Rais Samia ameeleza kutoridhishwa na kasi ndogo ya ujenzi wa mradi huo, na amemtaka mkandarasi kuongeza kasi na kuacha visingizio.

Amewahakikishia wananchi kuwa mradi huo pamoja na miradi mingine inayotekelezwa na Serikali katika maeneo mbalimbali nchini itakamilishwa kama ilivyopangwa na pale ambapo mkandarasi atachelewesha hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.

Mhe. Rais Samia pia amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala Wilayani Kinondoni ambapo pamoja na kupokea maelezo ya Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Zavery Peter Benela amewatembelea wagonjwa wanaopatiwa matibabu ya nje na waliolazwa wodini.

Mhe. Rais Samia ametoa msaada wa shuka 200 kwa ajili ya wagonjwa na amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itachukua hatua zaidi kutatua tatizo la upatikanaji wa dawa, kuboresha maslahi ya Madaktari na Wauguzi na kuboresha mazingira ya hospitali hiyo.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka Watanzania wote kuendelea kuchukua tahadhari zinazoshauriwa na wataalamu kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Korona (Covid-19).