November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungunza na Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Meru wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za sekta ya ardhi katika mkoa wa Arusha leo tarehe 1 Juni 2021. (Picha na Munir Shemweta).

Waziri Lukuvi afuta waraka unaowazuia madiwani

Na Munir Shemweta,WANMM-ARUSHA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amefuta waraka namba moja unaowaondoa madiwani kushiriki katika shughuli za uidhinishaji mipango ya uendelezaji miji katika maeneo yao uliotolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi nchini.

Kabla ya kutolewa waraka huo mpya Madiwani kupitia kamati zao za mipango miji walikuwa ndiyo wenye mamlaka ya kubariki mipango ya uendelezaji miji katika halmashauri husika kupitia vikao vyao vya robo mwaka na waraka mpya unataka shughuli hizo sasa kufanywa na wataalamu wa mipango miji kwa kushirikisha sekta mbalimbali kama vile sekta za maji, barabara, umeme nk.

Lukuvi alifanya maamuzi hayo leo tarehe 1 Juni 2021 katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Meru wakati akizingumza na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kusikiliza na kutatua kero za ardhi katika mkoa wa Arusha.

Alisema, kwa sasa waraka huo ameufuta mpaka utakapotolewa mwingine wenye maelekezo yatakayokuwa na tija na kusisitiza kuwa haiwezekani kuwaondoa madiwani kupitisha mipango ya uendelezaji miji katika halmashauri zake kwa kuwa mamlaka ya upangaji bado ziko chini halmashauri.

“Nimeamua kuufuta waraka namba moja unaokataza madiwani kupanga mipango ya uendelezaji miji katika halmashauri zenu, huwezi kuwa na halmashauri inayoshindwa kupitisha au kubariki mipango ya wilaya katika matumizi ya ardhi” alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, wataalam wa mipango miji katika ofisi za ardhi za mikoa waendelee kuwa washauri kwa kamati za mipango miji katika mabaraza ya madiwani.

“Kama vibali vya ujenzi tuliwaondoa na kupanga pia tuwaondoe, mtafanya kazi gani ? hiyo haiwezekani, kwa sasa muongozo unaokuja kamati za ardhi na makazi zitapatiwa ufafanuzi wa namna bora ya matumizi ya ardhi na baadaye kupelekwa kwa maafisa mipango miji.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ametangaza kufutwa kwa shamba la Valeska lenye ukubwa wa ekari 4,087 katika halmashauri ya wilaya ya Meru mkoani Arusha.

Lukuvi alitangaza uamuzi huo baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufuta shamba hilo kufuatia kuombwa kufanya hivyo na Waziri wa Ardhi. Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema halmashauri ya wilaya ya Meru itawajibika kulipa fidia katika maeneo yanayohitaji fidia ambapo kwa mara ya mwisho fidia ilikuwa milioni 394.10.

Waziri Lukuvi alianisha matumizi ya shamba lililofutwa kuwa ni ekari 1500 kugawiwa kwa vijiji vitatu vya Kwaugoro, Valeska na Maloloni na kuongeza kuwa ekari 1028 zitatumika kwa shughuli za kilimo na ekari 1559 kwa matumizi mbalimbali kama makazi na biashara.