November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro,Vicky Nsilo Swai

CCM yamlilia mwanasiasa mkongwe Vicky Swai

Na Mwandishi wetu,TimesMajira,Online

CHAMA cha Mapinduzi CCM ,kimepokea kwa masikitiko kifo cha mwanasiasa mashuhuri aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho mkoani Kilimanjaro Vicky Swai kilichotokea Mei 31 ,2021 moshi mkoani Kilimanjaro.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho,Shaka Hamdu Shaka  ilisema Mwenyekiti wa Chama hicho  ambaye ni Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemtaja marehemu Vicky Nsilo Swai kama mwanasiasa mahiri ,mpambanaji  mwenye msimamo thabiti wakati wa uhai wake.

Alisema pia  Vicky alikuwa mstari  wa  kupigania usawa wa kijinsia ,utu na adhi ya mwanamke.”Marehemu mama Vicky alitumia sehemu kubwa ya uhai wake kuwaunganisha wanawake wa Tanzania na kuwahimiza katika kushiriki shughuli za maendeleo kisiasa ,kijamii na kiuchumi,”Ilisema sehemu ya taarifa hiyo

Aidha taarifa hiyo ilisema Mama Vicky amewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Kilimanjaro,pia akiwa mke wa Muasisi wa Chama hicho  marehemu Asanterabi  Zephaniah Swai alishiriki katika harakati za ukombozi wa Tanganyika pamoja na kusiadia ukombozi wa mataifa mengine kusini mwa Bara la Afrika.

“Miongoni mwa sifa kubwa alizowahi kuwa nazo Marehemu Vicky Swai,ni uaminifu ambapo amewahi kuhifadhi viatu vya mpigania uhuru na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Afrika Kusini Hayati Mzee Nelson Mandela kwa miaka 33 kuanzia mwaka 1962 vilipoachwa na mpiganaji huyo wa ANC kwa familia ya Mzee Swain a kuvikabidhi kwake mwaka 1995 akiwa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kusini,”alisema Samia Suluhu Hassan katika  taarifa yake.

MWISHOOO