Na Esther Macha, TimesMajira,Online,Mbarali
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ,Twalibu Lubandamo amewataka wazazi na walezi wilayani humo kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanatimiza mahitaji muhimu ya watoto wao wakati wa masomo ikiwemo ununuzi wa sare za shule na uchangiaji wa michango ya shule na sio kuiachia Serikali.
Akizungumza juzi wakati wa mkutano wa baraza la Mamlaka ya Mji mdogo Rujewa ambalo liliwajumuisha wenyeviti wa vitongoji na viongozi wa mamlaka amesema kuwa bado kuna baadhi wazazi ambao hawajui wajibu wa kuhudumia watoto vifaa ya shule na kufikiri kuwa ni wajibu wa serikali pekee .
Lubandamo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Itamboleo alisema kuwa kutokana na dhana ya elimu bila malipo baadhi ya wazazi wamekuwa hawajishughulishi na maendeleo ya elimu ya Watoto wao ikiwa ni Pamoja na kugomea kununua mahitaji muhimu yanayopaswa kufanywa na mzazi mwenyewe na badala yake wanaitegea Serikali pekee.
Hata hivyo amesema kuwa wapo baadhi ya wazazi wanawaruhusu wanafunzi kwenda shuleni bila ya sare za shule wala daftari na kugomea kuchangia madawati na michango mingine ya shule inayokuwa inahitajika.
“Dhana ya elimu bila malipo imepokelewa vibaya na baadhi ya wazazi kwani hawasikii wala kuelewa jambo lolote linalohusu michango ya shule kama vile madawati ya kukalia mbaya zaidi wanamtuma mtoto shule bila daftari wala sare za shule eti atazikuta huko huko serikali itamnunulia” alisema Mwenyekiti huyo.
Aliongeza kuwa ili kukabiiana na hali hiyo elimu zaidi inapaswa kutolewa kwa wazazi na walezi kuhusu mfumo wa elimu bila malipo ikiwa ni pamoja na wazazi kujenga utamauni wa kutembelea mahali anaposoma mtoto ili kujionea miundombinu iliyopo.
Kwa upande wake Katibu tawala la Wilaya ya Mbarali, Michael Semindu akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Reuben Mfune alisema mali na changamoto ya upungufu wa madawati unaoikabili Halmashauri hiyo pia inauhitaji mkubwa wa vyumba vya madarasa.
Amesema kwa mwaka wa masomo wa 2020/2021 ni madarasa 46 yamejengwa katika Wilaya hiyo hivyo kuhitajika madarasa zaidi ya 100 kwa mwaka wa masomo ujao hivyo ili kukamilisha hilo nguvu za ziada zinahitajika kati ya wadau na wazazi.
Ameongeza kuwa kutokana na upungufu wa madarasa pamoja na madawati jambo hilo limepelekea uwepo wa utoro mkubwa wa wanafunzi Pamoja na mimba jambo ambalo limeshindwa kupatiwa ufumbuzi kwa wahusika kumalizana kifamilia.
Awali akifungua mkutano wa Baraza hilo, Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Rujewa , Chameta Godigodi amesema kuwa Mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto chache ikiwemo kutokamilika kuwa mamlaka kamili hivyo kushindwa kutatua baadhi ya mahitaji kama mamlaka.
Amesema changamoto nyingine ni urejeshwaji wa asilimia chache ya mapato kwenye Mamlaka hiyo kutoka Halmashauri tofauti na makusanyo waliyonayo hivyo kuanyima fursa ya kutatua mahitaji muhimu kwa wananchi ikiwemo ukarabati wa miundombinu ya barabara, madarasa na madawati.