November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Njombe awashauri wananchi kujikita kwenye ufugaji kwani unalipa

Na Omary Mtamike,TimesMajira online,Njombe

MKUU wa Wilaya ya Njombe Ruth Msafiri amewataka wananchi wa Mkoa wa Njombe na Tanzania kwa ujumla kuingia kwenye shughuli za ufugaji kwa sababu unalipa na hautumii muda mwingi wa mfugaji.

Kiongozi wa timu ya wataalam wa mradi wa “CIAT” An Notenbaert (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri mbegu za malisho aina ya “Brachiaria” baada ya kufurahishwa na jitihada zilizooneshwa na kiongozi huyo kwenye tasnia ya ufugaji kwa ujumla wakati wa ziara ya timu ya wataalam, wafugaji na wazalishaji wa malisho kutoka mikoa ya Mbeya, Njombe,Tanga na Kilimanjaro iliyofanyika mkoani Njombe.

Msafiri ameyasema hayo shambani kwake baada ya kutembelewa na timu ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wawakiloshi wa mradi wa utafiti wa malisho unaozingatia utunzaji wa Mazingira (CIAT) na wafugaji na wazalishaji wa malisho kutoka mikoa ya Njombe, Tanga na Kilimanjaro .

“Mfano mimi hapa kila mwezi kwa ng’ombe jike niliyenaye hapa nina uhakika shilingi 200,000 na zaidi kwa mwezi na kinyesi cha ng’ombe hawa natumia kama mbole kwenye mashamba yangu ambayo tangu nianze ufugaji sijawahi kutumia mbolea za kisasa” amesema.

Aidha Msafiri amebainisha ukosefu wa soko la uhakika la maziwa kama moja ya changamoto zinazowakabili wafugaji mkoani Njombe ambapo amesema kuwa bei ya lita moja ambayo viwanda vinanunua maziwa kwa wafugaji ipo chini ulilinganisha na bei iliyopo mtaani.

Akizungumzia kuhusu uhimilishaji Msafiri ameisifia teknolojia hiyo kwa kurahisisha upatikanaji wa ng’ombe bora na wa kisasa ambapo aliiomba Wizara kupeleka wataalam wa kutosha wa teknolojia hiyo hasa kwenye ngazi ya kata wanakopatikana wafugaji wengi.

“Bado wataalam wetu kwa upande wa hii teknolojia ni wachache na hata mimi hapa kwangu ng’ombe ameingia joto mara mbili lakini mtaalam ni mmoja na anatoka mbali hivyo kila akifika hapa anakuwa amechelewa na hapo natakiwa kusubiri tena mwezi mwingine” alisisitiza Msafiri.

Kwa upande wake kiongozi wa timu ya wataalam wa mradi wa “CIAT” An Notenbaert mbali na kufurahishwa na kazi nzuri iliyofanywa na wanifaika wa mradi huo, amewapongeza wafugaji wa Mkoa wa Njombe waliowezeshwa na mradi huo kwa kazi kubwa waliyofanya ambapo alimpa zawadi ya mbegu za malisho ya “brachiaria” aina ya kobra, mulato II na Cayman Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri baada ya kuvutiwa na jitihada zake katika tasnia ya ufugaji kwa ujumla.

Mwalimu Joseph Kihongo kutoka shule ya Msingi Ikando (kushoto) akiwaeleza wataalam, wafugaji na wazalishaji wa malisho kutoka mikoa ya Mbeya, Njombe,Tanga na Kilimanjaro kuhusu mradi wa ulimaji malisho ya mifugo unaotekelezwa shuleni hapo wakati wa ziara ya timu hiyo iliyofanyika mkoani Njombe

Akizungumza kuhusu umuhimu wa ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) Dkt. Jonas Kizima amesema kuwa ni lazima wafugaji wabadilike na kutambua kuwa ufugaji wa ng’ombe wengi bila kutenga maeneo ya kuzalisha malisho hauna tija na unasababisha migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa Ardhi.

“Wafugaji ni lazima wajue kuwa ili ng’ombe aweze kuzalisha maziwa kwa wingi anapaswa kupewa malisho bora na ndio maana unaona wakati wa kiangazi uzalishaji wa maziwa hupungua hadi asilimia 50 kwa sababu wafugaji wengi hutegemea malisho yanayostawi wakati wa masika hivyo sasa ni lazima tubadilike kwa sababu haya malisho pia imeshakuwa ni biashara nzuri sana hata kwa mtu asiyefuga” Amesisitiza Dkt. Kizima

Kwa upande wa mmoja wa wafugaji waliotembelewa na timu hiyo, Juliana Mlagala amesema kuwa ziara hiyo imemuongezea tija baada ya kujifunza mambo mbalimbali ambayo alikuwa akikosea hapo awali.

“Ufugaji kwangu ndio kila kitu kwa sababu ninasomesha watoto na kufanya shughuli zote za maendeleo na leo nimejifunza zaidi kuwa sisi wafugaji hatupaswi kugeuza mifugo yetu kama dhamana ya kukopa bali tuitumie kupata fedha ambazo zitatufanya tukidhi mahitaji yetu” alihitimisha Mlagala.