Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) liimarishe usimamizi utakaosaidia vyuo kutoa elimu inayozingatia viwango vya ubora na vyenye kukidhi mahitaji ya soko ya ajira.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati akifungua Maonesho ya Pili ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika uwanja wa Jamhuri huku akisema ni wajibu wa vyuo hivyo kuhakikisha vinatoa elimu bora ili kazi za vijana wanaotoka katika vyuo hivyo ziwe bora na zenye kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.
Aidha amezitaka taasisi za vyuo hivyo kufanya tathimini na kujipima ili kuona ni kwa namna gani zinaweza kutoa Elimu bora inayokidhi mahitaji ya sasa ya soko la ajira na kutoa fursa kwa vijana kujiajiri.
Kwa mujibu wa Majaliwa, ulimwenguni kote elimu na mafunzo ya ufundi na ufundi stadi hujulikana kwa mchango wake mkubwa katika ukuaji wa maendeleo ya viwanda, uchumi na ustawi wa jamii.
“Kwa upande wa Serikali itaendelea kuweka sera ambazo zinatoa fursa kwa wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta ya elimu na hivyo, kuunga mkono juhudi za kuliletea Taifa maendeleo. ” Amesema na kuongeza kuwa
“Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za umma na binafsi ambazo zinatoa Elimu na Mafunzo ya Ufundi hapa nchini.”
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa Wizara itaendelea kuhakikisha inatoa elimu ya mafunzo ya ufundi kwa kuzigatia mahitaji ya soko ya kipindi husika na kuwaandaa vijana kwa siku zijazo.
Aidha amesema lengo la maonyesho hayo ni kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa mafunzo ya ufundi ili kujionea mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa nchi huku akisema serikali inajihidi kutoa mafunzo yanayoebdana na mahitaji ya wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la NACTE Profesa John Kondoro Amesema mafunzo ya elimu ya ufundi kwa fani mbalimbali hivi yanatolewa katika vyuo 430.
Aidha Amesema NACTE kwa kushirikiana na wadau wengine wanaendelea kusimamia utoaji was mafunzo kuhakikisha Elimu ya ufundi inatolewa kwa ubora unaotakiwa ili iweze kukidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Maonyesho ya pili ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi yameanza Mei 28 na yanayarajiwa kuhitimishwa Juni 2 mwaka huu ambapo katika maonyesho hayo vijana wa kitanzania wanaonyesha ufundi wa aina mbalimbali kutokana na mafunzo wanayopata vyuoni.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa