Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online, Tanga
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021, Luteni Josephine Paul Mwambashi amewataka vijana kuitumia vizuri teknolojia hususani mitandao ya kijamii kuleta matokeo chanya na kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza kuharibu mfumo wa utamaduni wa Taifa.
Luteni Josephine ameyasema hayo wakati akizindua kituo cha Sayansi jiji la Tanga cha PROJECT INSPIRE, ambapo alieleza kuwa kumekuwepo na matumizi mabaya ya maendeleo ya teknolojia hususani mitandao ya kijamii.
“Hili linawahusu sana vijana na watoto wetu, sasa hivi Dunia ipo kiganjani mwetu, mfumo wa tabia kwa kiwango kikubwa unabadilishwa na teknolojia hususani mitandao ya kijamii inaharibu sana utamaduni wetu pindi inapotumika vibaya,”amesisitiza.
Ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kushirikiana na wadau kwa kufanikiwa kujenga kituo hicho kikubwa cha Sayansi Afrika Mashariki.
“Niipongezee halmashauri hii na wadau waliofanikisha kujengwa kwa kituo hiki, ninaamini kitasaidia wanasayansi wa Tanga na Tanzania nzima kwa ujumla, hivyo kitumike kwa malengo yaliyokusudiwa,”amesisitiza Luteni Josephine.
Awali akitoa taarifa ya kituo hicho Ofisa Utekelezaji, Rukia Hamad amesema, mpaka sasa kituo hicho kimekamilika na kwamba kimefikia asilimia 95 huku kikigharimu zaidi ya shilingi milioni 250.
Amesema kuwa, nje ya kufundisha wanafunzi masomo ya Sayansi lakini pia kituo hicho kinatoa fursa kwa Walimu wa masomo ya TEHAMA,sayansi, uhandisi na mahesabu kujiendeleza kitaaluma ili kuboresha mbibi za ufundishaji wao kulingana na viwango vya kidunia.
Amesema, lengo la kituo hicho ni kuendeleza ubora wa elimu ya sayansi na teknolojia kwa kuongeza ushiriki wa wanafunzi.
“Lakini pia tumepanga kuongeza uwezo wa wanafunzi kuelewa dhana na nadharia wanazofundishwa darasani kwa kuwapatia njia mbadala za kujifunzia kwa kutumia TEHAMA ,”amesema.
Amesema, wametengeneza maabara ya TEHAMA inayowawezesha wanafunzi,walimu na vijana kujifunza jinsi ya kutumia digitali kuzifahamu sheria za TEHAMA na kubuni mifumo na vifaa mbalimbali vinavyotatua matatizo na kuwatengenezea ajira.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa