Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Morogoro
WAZALISHAJI, wauzaji, wasambazaji na wadau wengine wa bidhaa za viungo mkoani Morogoro wamepatiwa mafunzo kuhusu uzalishaji bidhaa zenye ubora na viwango vinavyokubali ili kupanua soko lao ndani na nje ya nchi.
Mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha kuondokana na uuzaji, usambazaji na uzalishaji wa viungo kwa nia ya kujikimu, bali wafanye biashara zenye tija na hatimaye waweze kushiriki katika uchangiaji wa pato la Taifa.
Hayo yamesemwa juzi eneo la Matombo mkoani Morogoro na Meneja Mafunzo na Utafiti wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Hamis Sudi Mwanasala, wakati wa mafunzo yaliyotolewa kwa wauzaji, wasambazaji, wazalishaji na wadau wa viungo ili wabadilike na kuondokana na uendeshaji wa shughuli zao kwa nia ya kujikimu.
Ametaja wadau hao kuwa ni wauzaji, wasambazaji na wazalishaji wa viungo ikiwemo iriki, mlalasini, karafuu na vinginevyo kutokana na mkoa huo kuwa na wazalisha na wadau wengi wanaojipatia kipato kupitia bidhaa hizo za viungo.
Mwanasala alisema; “Serikali baada ya kutambua kwamba wajasiriamali wana mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi hii, wanasisitizwa wabadilike kuzalisha kwa wingi bidhaa zenye ubora ambazo zitaingia kwenye soko ndani na nje ya nchi bila vikwazo vya kibiashara.”
Amesema shirika hilo linawataka wafuate viwango, lakini pia kanuni bora za afya na mazingira. Kupitia mafunzo haya pia alisema maofisa wa shirika hilo waliwapatia washiriki elimu juu ya usajili wa majengo ya bidhaa za vyakula na vipodozi.
Ameongeza kuwa awali majukumu ya usajili majengo ya bidhaa za vyakula na vipodozi yalikuwa yakitekelezwa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), lakini kwa sasa yanafanywa na TBS.
Amefafanua kwamba Shirika hilo kati ya majukumu yake makuu ni kutoa mafunzo yanayohusu viwango na ubora wa bidhaa, hivyo kinachofanyika kwa wauzaji, wasambazaji na wazalishaji wa bidhaa hizo za chakula (viungo) ni sehemu ya utekelezaji majuku yake.
Amesema wakati mwingine mafunzo ya aina hiyo yanaombwa na wadau ili kupatiwa elimu kuhusu shughuli zao ili ziweze kuwa na tija, kwa maana ya kuongeza thamani ya bidhaa zao na kufuata kanuni bora za uzalishaji na uendeshaji wa shughuli zao.
“Sisi kama shirika tunawajibika kutoa mafunzo na hilo ni jukumu letu na wakati mwingine tunaalikwa na tunashiriki kutoa elimu kupitia maonesho ya Nane Nane, Saba saba na wakati mwingine taasisi nyingine kama SIDO na Tantrade zikiandaa mafuzo zinatuliaka ili tuweze kutoa elimu,” amesema.
Alisema huko nyuma uzalishaji wa bidhaa nyingi za vyakula, ulikuwa uzalishaji wa kufikirika, lakini sasa wanatakiwa kuja kibiashara na ili kuzalisha kibiashara lazima bidhaa hizo ziwe na ubora unaokunbalika, ziwe na viwango vinavyokubalika ili waweze kuingia kwenye soko kwa kujiamini.
Aliwataka wajasiriamali hao kutambua kwamba wao ni watu wenye mchango mkubwa katika uchumi wa nchi. “Kwa hiyo mnapopata elimu ambayo itawasaidia kuboresha bidhaa zenu mtaongeza thamani ya bidhaa zenu na zitakubalika katika masoko ya ndani na nje,”alisema Mwanasala.
Baadhi ya wadau walioshiriki mafunzo hayo ni SIDO na Tantrade. Kwa upande wa Tantrade walitoa elimu kuhusiana na masuala ya masoko hususan masoko ya nje ya vyakula, kutokana na bidhaa za viungo kuhitajika sana huko.
Kwa upande wa SIDO walitoa elimu kuhusu uchakataji na uzalishaji bora wa vyakula.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi