April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto

Wakiri kumuua mwenzao kwa gobore

Na Doreen Aloyce, Dodoma

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma limefanya msako mkali wa kukamata wahalifu wa makosa mbalimbali ambapo linawashikilia watuhumiwa wawili waliohusika na mahuaji pamoja na silaha mbili aina ya gobore zilizotumika katika mauaji hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gilles Muroto amesema kuwa, tukio hilo la mauaji lilitokea katika kijiji cha Nhinhi Wilaya ya Chamwino ambapo watuhumiwa wawili Saimon Kikoti (36) na mwenzake George Mhando (44) walihusika na mauaji ya kumuua Samsoni Kikoti (56) kwa kutumia silaha aina ya gobore majira ya saa moja usiku.

Aidha, amesema kuwa baada ya kuhojiwa kwa watuhumiwa hao walikiri kuhusika katika mauaji kwa kutumia silaha huku ikielezwa chanzo na sababu za kujichukulia sheria mkononi ni kwa kumtuhumu marehemu kuwa ni mwizi wa mifugo kwa muda mrefu.

‘’Niwasihi watu muache kujichukulia sheria mkononi kama mtu anatuhumiwa kwa makosa ya uhalifu mtoe taarifa katika kituo cha polisi ili waweze kukamatwa na kufanyiwa uchunguzi dhidi ya makosa yao,”amesema Kamanda Muroto.

Muroto amesema, katika msako mwingine jeshi la polisi limewakamata jumla ya watu 23 wakicheza kamari kinyume na sheria katika mitaa ya Bahi road na Makulu Tarafa na Wilaya ya Jiji la Dodoma.

Amesema kuwa, katika msako wa tarehe 25, mwaka huu mtaa wa Amani kata ya Chang’ombe walikamatwa Maulid Shaka (33) mkazi wa Chang’ombe na wenzake 6 wakijihusisha na vitendo vya uhalifu wa uporaji kwa kutumia usafiri wa pikipiki tofauti.

‘’Watuhumiwa walikuwa wanatafutwa kwa makosa hayo, mbinu wanayotumia kupakia abiria nyakati za usiku na wengine wanawafuata nyuma na kuwavamia huku wakiwapora wakati abiria anashushwa au akiwa njiani,”amesema.

‘’Wakati tukiendelea na msako kila sehemu tulifanikiwa kukamata pikipiki mbili ambazo wamekuwa wakizitumia kufanyia uhalifu huo ambazo ni MC.601 BQL HAOJUE na MCL.154 CJJ BOXER,”amesema Muroto.