November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watuhumiwa 20 wanaswa Dar

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam wamefanikiwa kukamata watuhumia 20 katika matukio mbalimbali ikiwemo la kukamata watu watano wakidaiwa kupora silaha katika nyumba ya Mkurugenzi wa Benki ya Azania.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam,SACP- Camillius Wambura amesema, jeshi hilo linaendelea kutoa onyo kwa wahalifu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu waache mara moja, kwani jeshi lipo imara na limejipanga vizuri kuhakikisha hali ya Jiji inaendelea kuwa shwari.

Amesema, Machi 18,2021, saa 8.00 usiku majambazi watano walivamia nyumba ya Mkurugenzi wa Benki ya Azania iliyopo Mbweni Mpiji na kuwashambulia walinzi wa kampuni ya SUMA JKT na kuwapora silaha aina ya Short Gun Pump Action ikiwa na risasi tano.

SACP Wambura amesema, jeshi hilo lilifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kukamata silaha hiyo, Mei 20,2021 na watuhumiwa watano waliohusika katika tukio hilo.

Aidha, katika tukio lingine polisi wanawashikilia watu watano kwa tuhuma za mauaji. Miongoni mwa watu wanaodaiwa kuuawa na majambazi hao ni pamoja na Issa Karim (33), Mkazi wa Mbezi, Mohamed Juma (31), Mkazi wa Mbezi Mwisho,Selemani Seif (34)Mkazi wa Mbezi Mwisho,Samsoni Joseph (32), Mkazi wa Mbezi na Ezekiel Kennedy Mkazi wa Mbezi.

“Mnamo Mei 8,2021 majira ya 8:05 usiku Mikocheni A watuhumiwa hawa walivamia katika baa iitwayo Imbizo na kumshambulia kwa mapanga na marungu mlinzi aliyefahamika kwa jina Regan Sylivester na kusababisha kufariki dunia papo hapo,”amesema

Amesema, watuhumiwa hao wanahusika na tukio la unyan’ganyi wa kutumia silaha Mabwepande ambapo mnamo Mei 7,2021 majira ya 9:00 usiku walivamia katika kituo cha kuuzia Mafuta cha MEXONS na kuwashambulia walinzi, wahudumu na wateja na kupora kiasi cha sh. 2, 440,000 na kisha kupora silaha aina ya Short Gun ya walinzi hao.

Pia SACP Wambura amesema, katika tukio lingine Jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa watano kwa kosa la uvunjaji wa nyumba usiku na kuiba.

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na baadhi ya mali walizoiba ikiwa ni pamoja na TV moja aina ya LG NCH 55 Flat screen,Simu mbili aina ya iphon, Laptop mbili aina ya Dell na Mouse nne za kompyuta.

Alitaja watuhumia hao kuwa ni pamoja na Abeid Said (41), Laurent Mwazembe(44), Ramdhani Mohamed, (31), Julias Mapunda, (34), Emmanuel Zongo (30) pia linawashikilia watu sita kwa tuhuma za uvunjaji maduka usiku na kuiba.

Watuhumiwa hao ni Kaburu Mohamed (30),Iddi Ally 30, Said Ramadhani (33), Lucas Danford (31), Shaban Bakari (33) na Khamis Bahati ( 38).

Alisema watuhumiwa hawa wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uvunjaji maduka nyakati za usiku katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam hususani katika mitaa ya Kariakoo na Ukonga Banana.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limefanikiwa kukamata magari manne na watuhumiwa wanne na kufanikiwa kukamata Pikipiki namba MC 136 CSA Boxer nyeusi iliyokuwa imeibiwa mei 15,2021 huko maeneo ya Kibamba shule na kupelekwa Gairo Mkoani Morogoro.